Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Arusha Mount Meru,Daktari Alex Ernesti akizungumza katika hafla hiyo
Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongela akizungumza katika hafla hiyo jijini Arusha (Happy Lazaro)
……………………………………………………………
Happy Lazaro, Arusha
HOSPITAL ya rufaa ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru imeanza kutoa huduma ya matibabu bure ya magonjwa mbalimbali ambayo itatolewa kwa siku tisa mfululizo hadi Desemba 9 ikiwa ni kusherehekea miaka 60 ya Uhuru .
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo,Daktari Alex Ernesti,ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa kambi ya huduma ya matibabu inayofanyika hospitali ya rufaa ya Mount Meru,na kusema kwenye kambi hiyo wapo madaktati bingwa 17 wa magonjwa mbalimbali ambao wanajitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata huduma hiyo.
Amesema kuwa, kutokana na wingi wa wagonjwa hospitali hiyo inaangalia uwezekano wa kuanzisha kambi hizo za matibabu kutolewa hadi ngazi za wilaya ili kuwezesha wananchi wengi kupata huduma hiyo kwenye maeneo ya karibu.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Arusha. John Mongela,amesema ,serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha huduma ya afya ambapo katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru kiwango cha hospitali ,Vituo vya afya na Zahanati vimeongezeka na vimeboreka sanjari na kuongezeka kwa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali.
Amesema kuwa,wakati wa Uhuru kulikuwepo madaktari wachache hospitali ,Vituo vya afya na zahanati chache lakini katika kipindi cha kuanzia Uhuru hadi sasa miaka 60 sekta ya afya imeboreka,ambapo katika kipindi cha miezi sita serikali imetoa fedha nyingi za kuboresha sekta hiyo.
Aliwaomba ambao hawajapata chanjo ya ugonjwa wa Uviko -19 kuhakikisha wanachanja ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Hata hivyo aliwataka wananchi kutoka maeneo mbalimbali mkoani Arusha kujitokeza kwa wingi katika kupata huduma mbalimbali na huku akiwataka kutumia fursa katika siku hizo kuelekea desemba 9.