Viongozi wa chama cha msingi cha ushirika Mlingoti Mashariki wilaya ya Tunduru wakipanda gari la Polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuingiza zaidi ya tani 10 za korosho chafu kutoka nje ya wilaya hiyo kwa lengo la kuuza kwenye minada.
Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha Ushirika Mlingoti Mashariki Seleman Makochela wa kwanza kulia na viongozi wengine wa chama hicho wakiwa chini ya ulinzi wa Polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuingiza kwenye maghala korosho chafu kutoka nje ya wilaya ya Tunduru katika operesheni za mazao zinazofanywa na kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na Mkuu wa wilaya Julius Mtatiro.
Baadhi ya viongozi na wajumbe wa bodi za vyama vya msingi vya ushirika wilayani Tunduru wakiangalia korosho chafu zilizoingizwa na viongozi wa chama cha msingi cha ushirika Mlingoti Mashariki kwa lengo la kuuza kwenye minada inayoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Sehemu ya tani 10 za Korosho chafu zilizoingizwa kwenye maghala ya chama cha msingi cha Ushirika Mlingoti Mashariki na viongozi wa Chama hicho kutoka nje ya wilaya ya Tunduru kwa lengo la kuuza katika minada ya korosho inayoendelea.
Picha zote na Muhidin Amri
………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Tunduru
VIONGOZI sita wa chama cha msingi cha ushirika(Amcos)cha Mlingoti Mashariki wilayani Tunduru akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Seleman Makochela, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakituhumiwa kuingiza korosho chafu kutoka maeneo ya nje ya Tunduru.
Korosho hizo ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu, ziliingizwa wilayani humo kwa lengo la kuuza kwenye minada inayoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro alisema hayo jana katika kikao chake na wenyeviti wa vyama vya msingi,waandishi,makalani,wajumbe wa bodi na viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu) ofisini kwake mjini Tunduru.
Alisema, viongozi hao wamekatwa juzi baada ya kuwepo kwa taarifa ya baadhi ya wafanyabiashara wamepanga njama za kuingiza korosho chafu kwenye soko la korosho bora zinazozalishwa wilayani humo.
Alisema, viongozi hao kwa kushirikiana na wafanyabishara ambao wanaendelea kutafutwa na vyombo vya dola wamehusika kuingiza zaidi ya tani 10 za korosho hizo kwenye maghala na vituo vya kukusanya korosho kwa lengo la kuchafua soko la zao hilo.
Aidha alisema, wanamshikilia mkazi wa kijiji cha Nandembo Eliza Ponera baada ya kukamatwa akiwa na magunia 27 ya korosho chafu nyumbani kwake akijiandaa kuingiza katika maghala ya vyama vya msingi.
Mtatiro alisema, hali hiyo ikiachwa bila kudhibitiwa itashusha uzalishaji,ubora na sifa za korosho za Tunduru na ameliagiza Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama, kuwatafuta watu waliohusika kuingiza korosho hizo na kusambaratisha mtandao wote unaojihusisha na vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa Mtatiro, vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya operesheni katika maghala mbalimbali na vitahakikisha korosho zinazolimwa katika wilaya ya Tunduru zinalindwa kwa gharama yoyote.
“hili ni jambo la kiuni na kifedhuli sana linalofanywa na baadhi ya watu wenye nia mbaya ya kuchafua zao la korosho zinazolimwa hapa Tunduru,mimi na kamati yangu ya ulinzi na usalama tutahakikisha watu wote waliohusika kuingiza korosho chafu tunawapata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria”alisema.
Katika hatua nyingine,Mtatiro amemtaka Afisa Ushirika wa wilaya hiyo kukifuta Chama cha Mlingoti Mashariki na kusitisha zoezi la kukusanya korosho za wakulima zilizokuwa zinafanywa na chama hicho, na kuagiza kazi hiyo ifanywe na Chama cha Mlingoti Magharibi.
Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, amewaonya Mameneja wa vyama vya ushirika katika wilaya hiyo,kutopokea korosho chafu kutoka kwa watu wasiofahamika na wenye nia ya kuhujumu zao hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu) Mussa Manjaule alisema,kitendo kilichofanywa na viongozi wa chama hicho ni kutaka kuhujumu uchumi wa wilaya hiyo na mkoa wa Ruvuma.
Amewataka viongozi wa vyama vya msingi,kuwa waadilifu na waaminifu katika utendaji wao na kutojihusisha na vitendo vinavyoweza soko la zao la korosho zinazolimwa katika wilaya ya Tunduru.