Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) (waliovaa vitambulisho) wakikagua risiti za Mfanyabiashara wa Mkoa wa Njombe aliyekuwa Kariakoo Dar es Salaam akinunua bidhaa za kwenda kuuza mkoani humo wakati wa zoezi la kuhamasisha wafanyabiashara kutoa risiti na wanunuzi kudai risiti
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) (waliovaa vitambulisho) wakikagua mzigo wa Mfanyabiashara wa Mkoa wa Njombe na kulinganisha na risiti alizopewa wakati wa zoezi la kuhamasisha wafanyabiashara kutoa risiti na wanunuzi kudai risiti. Zoezi hilo limeanza leo mkoani Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA TRA).
**************
Na Mwaandishi wetu
Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kampeni ya kuhamasisha matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFD) ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wanunuzi kudai na kukagua risiti kila wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.
Akizungumza wakati wa kampeni hiyo iliyoanza katika eneo la Kariakoo Dar es Salaam, Msimamizi wa Kitengo cha EFD wa Mkoa wa Kikodi Kariakoo Bw. Hamidu Shaban alisema kuwa, zoezi hilo ni endelevu na linafanyika katika maeneo yote ya Dar es Salaam.
“Tunafanya zoezi hili katika mkoa mzima wa Dar es Salaam kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti kuanzia kwenye mizigo yote inayozalishwa viwandani na kupelekwa madukani inauzwa kwa risiti na kuhakikisha wale wanaonunua bidhaa wanadai risiti,” alisema Bw. Shaban.
Bw. Shaban amezitaja adhabu za kutokutoa na kudai risiti kuwa ni shilingi milioni 1,500,000 hadi 4,500,000 kwa wafanyabiashara wasiotoa risiti za EFD na wanunuzi wasiodai risiti, adhabu ni shilingi 30,000 hadi shilingi milioni 1,500,000.
Rehema Mbilinyi ni Mfanyabiashara wa Kariakoo ambaye amefurahishwa na zoezi hilo linalofanyika la kuhamasisha matumizi ya EFD ambapo ameiomba Serikali kugawa makundi ya wafanyabiashara wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kuweka viwango tofauti tofauti vya VAT ili kuondoa tatizo la baadhi ya wafanyabiashara kutoa risiti pungufu au kutokutoa kabisa kwa kuogopa kuingia kwenye VAT.
“Kampeni hii ni nzuri lakini mimi naona kuna haja ya Serikali kutoza kodi ya VAT kwa kugawa makundi kwa mfano, wale wafanyabiashara wakubwa wawe na asilimia 18 kama kawaida, wafanyabiashara wa kati watozwe asilimia 10 na wasajiliwa wapya wa VAT waanze kwa asilimia 5. Hii itasaidia kupunguza tatizo la kutokutoa risiti au kutoa risiti pungufu,” alieleza Rehema.
Kwa upande wake, Sylivanus Nyigu ambaye pia ni mfanyabiashara wa Kariakoo, licha ya kuisifia kampeni hiyo, amesema zoezi hilo litasaidia kuondoa mapungufu yanayojitokeza kwenye suala zima la kutoa na kudai risiti na kuyatafutia ufumbuzi.
Mamlaka ya Mapato Tanzania imekuwa na utaratibu wa kufanya kampeni za mara kwa mara kwa lengo la kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi, kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za EFD pamoja na kuwakumbusha walipakodi kulipa kodi kwa wakati.