Baadhi ya wafanyakazi wa NSSF wakiandikisha wanachama wapya kutoka sekta isiyo rasmi wakati wa Maonesho hayo.
Julie Sowani ambaye ni mjasiriamali akijaza fomu ya kujiunga kuwa mwanachama wa NSSF baada ya kupata elimu ya hifadhi ya jamii kutoka kwa wafanyakazi wa NSSF wakati wa Maonesho ya 21 ya Nguvu Kazi/Jua Kali ya Afrika Mashariki 2021 yanafanyika katika uwanja wa Rock City Mall Jijini Mwanza.
Baadhi ya wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakiendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wajasiriamali ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba kwaajili ya maisha yao ya baadaye. Elimu hiyo inaendelea kutolewa katika Maonesho ya 21 ya Nguvu Kazi/Jua Kali ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika uwanja wa Rick City Mall jijini Mwanza.
********************
Na MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, ametoa wito kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutumia Maonesho ya 21 ya Nguvu Kazi/Jua Kali Afrika Mashariki kuandikisha wanachama wapya kutoka sekta isiyo rasmi ili waweze kuwa wanachama wa Mfuko huo na kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF.
“Nafurahi kusikia mpaka sasa wameshandikisha wanachama kama 230 lakini wamejiwekea malengo mpaka maonesho haya yanaisha wawe wameshaandikisha wanachama 1000,” alisema.
Waziri Jenista alisema hayo alipotembelea banda la NSSF katika maonesho hayo yanayofanyika jijini Mwanza, na kuongeza kuwa maonesho makubwa kama hayo ni muhimu kwa NSSF kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba.
“Katika maonesho makubwa kama haya yamekutanisha zaidi ya watu 1000, wenzetu wa Afrika Mashariki watajifunza jinsi gani Mfuko unafanyaka kazi, lakini hata Watanzania waliopo hapa watajifunza yale ambayo yanafanyika ndani ya NSSF, suala la msingi ni utekelezaji wa majukumu ya Mfuko kisheria na kuchangamkia fursa ya maonesho haya kuweza kuandikisha wanachama wapya ambao wapo katika sekta isiyo rasmi na kuingia katika Mfuko kama wanachama,” alisisitiza Waziri Jenista.
Aidha, Waziri Jenista alitoa wito kwa wajasiriamali waliopo katika maeneo mbalimbali nchini, kuutumia Mfuko wa NSSF kama sehemu ya kujiwekea akiba itakayo wawezesha kunufaika na mafao mbalimbali likiwemo la uzee.
“Ninatoa wito kwa wajasiriamali wote nchini, kuutumia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kama sehemu kujiwekea akiba itakayo wawezesha kunufaika na mafao mbalimbali likiwemo la uzee,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Kahensa, alisema NSSF inatoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wa makundi mbalimbali hasa wale waliopo katika sekta isiyo rasmi.
“Kupitia maonesho haya NSSF imekuwa ikitoa elimu ya hifadhi ya jamii na kufanya uandikishaji kwa wajasiriamali wanaoshiriki ili waweze kuchangia kwa ajili ya kesho yao pindi watakapopata majanga kwani kufanya hivyo kuna faida kubwa kwenye maisha yao ya sasa na baadaye,” alisema Kahensa.
Maonesho haya ya 21 ya Nguvu Kazi/Jua Kali ya Afrika Mashariki 2021 yanafanyika katika uwanja wa Rock City Mall Jijini Mwanza yakiwa na Kauli Mbiu isemayo: Kuhamasisha Ubora na Uvumbuzi ili kuongeza ushindani wa Wafanyabiashara wadogo na wa kati wa Afrika Mashariki na kuinuka kiuchumi baada ya janga la UVIKO 19