Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (aliyevaa kofia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali (aliyevaa miwani) jana wakikagua miundombinu ya ujenzi wa madarasa shule ya sekondari Nkasi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti(aliyevaa kofia) akizungumza na madiwani wa Nkasi kwenye mkutano wa hadhara jana mjini Namanyele ambapo alieleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo uliochukua muda mrefu bila kukamilika.
Sehemu ya majengo ya hospitali ya wilaya ya Nkasi ambayo yalikaguliwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambapo alieleza kutoridhishwa na kasi ndogo ya ujenzi licha ya serikali kuu kutoa fedha shilingi Bilioni 2.3 hadi sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza na wananchi wa Namanyele wilaya ya Naksi jana ambapo alisema atachukua hatua kwa watendaji waliokwamisha ujenzi wa miradi ya hospitali za wilaya Nkasi, Kalambo, Mtowisa na Manispaa ya Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (aliyevaa kofia ) akizungumza na walimu shule ya sekondari Mtenga wilaya ya Nkasi jana mara baada ya kukagua ujenzi wa madarasa chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
………………………………………………………………..
Madiwani wa halmashauri za mkoa wa Rukwa wametakiwa kuhakikisha miradi ya ujenzi wa hospitali za wilaya unakamilika kwa viwango kutokana na serikali kutoa fedha nyingi .
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alitoa agizo hilo jana (06.12.2021) mjini Namanyele wakati wa mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Posta ambapo alisema haridhishwi na kasi ndogo ya utekelezwaji wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Nkasi.
“Siridhishwi namna miradi ya afya inavyotekelezwa Nkasi na katika wilaya zingine za Sumbawanga na Kalambo. Serikali ilileta fedha mwaka 2019/20 hadi leo miradi haijakamilika na hakuna maelezo yaliyonyooka” alisema Mkirikiti
Mkirikiti aliwaeleza wananchi hao kuwa amebaini ushirikishwaji hafifu wa madiwani kwenye utekelezaji wa miradi ya afya hatua inayopelekea wananchi kutopata huduma kwani wawakilishi wao hawajui kinachoendelea kwenye halmashauri zao.
Aliongeza kusema hawezi kukubali kuona miradi hiyo ikikwama kutekelezwa kwenye halmashauri wakati Rais ameweka viongozi ambao ni Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi .
“Mkurugenzi Nkasi ni mpya, DC ni mpya Tunataka hospitali ikamilike lakini nao sasa wameanza kutoa stori kila siku hakuna kipya kinachoelendelea na fedha naambiwa zimeisha majengo hayajakamilika. Sitokubali hali hii”alisema Mkirikiti huku wananchi wakishangilia kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa.
Alitaji miradi ya ujenzi wa hospitali za wilaya iliyokwama kukamilika kuwa ni hospitali ya wilaya ya Nkasi, hospitali ya wilaya ya Kalambo iliyopo Matai, hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga iliyopo Isofu na hospitali ya wilaya ya Sumbawanga iliyopo Mtowisa.
“Hivi mlikuwa wapi niyi madiwani hata miradi hii ya hospitali inakwama . Je mlifungwa macho na midomo. Fedha zilikuja lakini miradi haijakamilika” alisema Mkirikiti
Alibainisha hatua za kudhibiti wote waliohusika na ukwamishwaji miradi hiyo kuwa “sasa hivi tunaanza kuchukua hatua kimya kimya kwani wengine naambiwa wamekula fedha na kuondoka kwenye maeneo yao. Tutawafuata huko huko “alisisitiza Mkirikiti.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Namanyele Diwani wa Kata ya Isunta Kudra Abeid alisema hospitali ya wilaya Nkasi inajengwa kwenye kata yake lakini hajawahi kujua ni kiasi gani cha fedha kimetumika kwani ilikuwa ni mradi unaosimamiwa na kutekelezwa na kikundi kidogo cha watu .
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali alisema mradi huo wa hospitali ya wilaya una mapungufu mengi ikiwemo tatizo la ukosefu wa taarifa muhimu za utekelezaji wake toka kwa Mkurugenzi ambapo amebaini halmashauri imemaliza fedha bila kazi kukamilika.
Takwimu za fedha zilizotolewa na serikali zinaonesha ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Nkasi ulianza mwaka 2019/20 ambapo shilingi Bilioni 2.3 zimetimika , hospitali ya Mtowisa (Bilioni 2.3), hospitali ya wilaya Kalambo (Bilioni 2.3) na hospitali ya Manispaa Isofu (Bilioni 1.5) tayari zimetumika licha ya majengo kutokamilika.
Mwisho