Mkuu wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora Sauda Mtondoo akipanda mti kwenye eneo la soko kuu la Igunga mjini katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru (Picha na Lucas Raphael, Igunga)
……………………………………………………..
Na Lucas Raphael,Tabora
Mkuu wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Sauda Mtondoo ametoa onyo kali kwa baadhi ya wananchi ambao wamekuwa na tabia ya kukata miti hovyo pasipo kufuata taratibu za kisheria za kutochukua vibali kutoka TFS.
Alitoa onyo hilo jana wakati wa zoezi la upandaji wa miti katika soko la mjini Igunga ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru hapa nchini.
Alisema pamoja na juhudi za serikali za kuhimiza wananchi kupanda miti kwa wingi lakini wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakikata miti hovyo katika maeneo ya mbalimbali ya wilaya ya Igunga pasipo kuwa na vibali serikalini na kusababisha baadhi ya maeneo kuwa na ukosefu wa miti.
“Ndugu zangu wananchi natoa onyo kali kwa mtu yoyote atakayebainika kukata miti hovyo pasipo kuwa na kibali serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kufuata taratibu wanapohitaji kukata miti lazima wawe na kibali kutoka TFS.
Aidha Mtondoo alizitaka taasisi za dini na mashirika mbalimbali kuhakikisha wanapanda miti za kutosha katika maeneo yao huku akizitaka kila kaya kupanda miti mitano na kuhakikisha wanaitunza miti hiyo.
Alisema lengo la kupanda miti ni kuboresha mazingira ikiwa ni pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake afisa usafi na mazingira wilaya ya Igunga Fredrick Mnahela alisema katika zoezi hilo la kuelekea miaka 60 ya uhuru halmashauri ya wilaya ya Igunga wamepanda miti 360 na kutoa maelekezo kuwa wananchi wapande miti na kufanya usafi kwenye maeneo yao.
Sambamba na hayo alisema idadi ya miti iliyopandwa msimu uliopita wa mwaka 2020/2021 walifanikiwa kupanda miti 97,784 ambapo alitaja maeneo yaliyopandwa ni taasisi, kaya na maeneo ya wazi, ikiwa lengo la upandaji wa miti kwa mwaka ni miti milioni moja na laki tano.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi walioshiriki zoezi la upandaji miti katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru George Lucas, Rehema Lucas na Asha Samwel walimshukuru mkuu wa wilaya kwa kutoa onyo la ukataji miti hovyo kwa kuwa kasi ya ukataji miti kwa wilaya ya Igunga imekuwa kwa kiwango kikubwa na kusema kuwa kauli ya mkuu wa wilaya itasaidia baadhi ya wananchi kutokata miti hovyo.