Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Desemba 7,2021 mara baada ya kusaini makubaliano ya utendaji baina ya Mabonde tisa ya maji na Wizara ya Maji, jijini Dodoma.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga,akisaini mkataba na Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya utendaji baina ya Wizara hiyo na Bodi za Maji za Mabonde iliyofanyika leo Desemba 7,2021 kwenye Ofisi ya Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga,akibadilishana mkataba na Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy mara baada ya kusaini makubaliano ya utendaji baina ya Wizara hiyo na Bodi za Maji za Mabonde iliyofanyika leo Desemba 7,2021 kwenye Ofisi ya Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma.
……………………………………………………
Na Alex Sonna, Dodoma
BODI ya Maji Bonde la Wami-Ruvu limejipanga kutekeleza mkataba wa utunzaji wa rasilimali maji kwa kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi wa kutosha kwenye bonde hilo huku likisisitiza zuio la shughuli za kibinadamu na umwagiliaji hadi pale maji yatakapokuwepo ya kutosheleza kwa matumizi hayo.
Kaimu Mkurugenzi Bodi hiyo, Mhandisi Elibariki Mmassy ameyasema hayo leo Desemba 7,2021 baada ya kusaini makubaliano ya utendaji baina ya Mabonde tisa ya maji na Wizara ya Maji, jijini Dodoma.
Amesema watahakikisha ndani ya mwaka mmoja mkataba huo unatekelezwa ipasavyo na agizo la kuzuia shughuli za kibinadamu za umwagiliaji kwenye bonde hilo litaendelea kuwepo hadi pale maji yatakapotosheleza kwa matumizi mengine.
“Sisi tunauhakika chini ya serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan rasilimali ya maji itatunzwa kwa ustawi wa vizazi vijavyo, mito iliyopo haiwezi kuongezeka na hakuna chemchem mpya bali ni maji yale yale ya miaka yote iliyokuwepo tangu dunia iumbwe hivyo ni lazima yatunzwe kwa kizazi cha sasa na kijacho.”
“Tunawahakikishia wadau wote waliopo bonde la Mto Wami-Ruvu maji watapata na watapata kwa uhakika, wateja wetu watapata maji kwa shughuli zao za kibinadamu, tunatoa rai maji yatumike kwa uangalifu mkubwa kwa kuwa bado mvua hazijaimarika, shughuli za kibinadamu zinakomeshwa na mifugo isifike kwenye vyanzo vya maji, ”amesema.
Kadhalika, amesema upotevu wa maji wakati wa masika utadhibitiwa ili kusaidia wakati wa miezi minne ya ukame wa bonde hilo.