Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Sophia Edward Mjema amefungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kupambana na Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu kwa Maafisa wa Uhamiaji, Waendesha Mashtaka wa Serikali, Polisi, Mahakimu na Maafisa Ustawi wa Jamii yaliyofanyika leo, 6/12/2021 wilaya ya Kahama- Shinyanga.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Sekretariet ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu na TRI (Tanzania Relief Initiative),yanalenga kuwajengea uwezo watendaji kujua mbinu za kupambana na biashara hii pamoja na namna ya kuisaidia jamii na wahanga wa biashara hii haramu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga na OCD kuchuku hatua za kisheria kwa watu watakaotambulika wanayafanya Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu mkoani Shinyanga. Awaomba wananchi kuungana kukomesha biashara hii kwa kutoa taarifa pale watakapobaini uhalifu huo.
Katibu wa Sekretariet ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu, SATC Seperatus Fella akizungumza na Watendaji wa Serikali wanaoshiriki kwenye Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa Kupambana na Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu. Mafunzo hayo yamefanyika leo, Desenba 6, 2021, Wilayani Kahama, Shinyanga.Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2020 hadi March 2021, jumla ya watanzania 163 ambao ni wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu waliokolewa na kati yao wahanga wawili (2) wameokolewa kutoka Iraq na Malaysia. Pia amesema jumla ya wahanga 15 kutoka nchi jirani ya Burundi, wameweza kuokolewa wakiwa wanatumikishwa hapa nchini na kurudishwa katika nchi yao.
Baadhi ya Watendaji na Wadau walioshiriki kwenye Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa Kupambana na Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu. Mafunzo hayo yamefanyika leo, Desemba 6, 2021 wilayani Kahama, mkoa wa Shinyanga.
Kamishna Msaidizi wa Sekretariet ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu, Ahmed Mwen-dadi amewataka watendaji wa Serikali walioshiriki katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa Kupambana na Kudhibiti Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, kutumia fursa kujifunza na kuelimisha jamii juu ya biashara hii haramu.