Mjiolojia kutoka PURA, Bw. Faustine Matiku akielezea jambo kuhusu sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini kwa washiriki waliotembelea banda la PURA kwenye Maonesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanayoendelea visiwani Zanzibar.
Mjiolojia kutoka PURA, Bw. Ebeneza Mollel akitoa maelezo kuhusu mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi kwa mshiriki wa Maonesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda visiwani Zanzibar aliyetembeleza banda la PURA.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji Tanzania (TEITI) Bi. Mariam S. Mgaya akiweka saini kwenye kitabu cha wageni kwenye banda la PURA katika Maonesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda visiwani Zanzibar. Pamoja naye ni Mjiolojia kutoka PURA, Ebeneza Mollel.
Afisa Uhusiano wa PURA Bi. Janeth Mesomapya akizungumza jambo Kaimu Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji Tanzania (TEITI) Bi. Mariam S. Mgaya aliyetembelea banda la PURA kwenye Maonesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanayoendelea visiwani Zanzibar. Pamoja nao ni Mjiolojia wa PURA, Bw. Ebeneza Mollel.
*****************************
Na Janeth Mesomapya
Maonesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanaendelea visiwani Zanzibar huku Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ikiwa miongoni mwa taasisi zinazoshiriki.
Kwa mujibu wa Mjiolojia wa PURA, Ebeneza Mollel, kwenye maonesho hayo PURA imejipanga kuwafikia wananchi na kuendelea kutoa uelewa wa masuala yahusuyo sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania pamoja na fursa zilizopo kwenye sekta husika.
Ameeleza kuwa uelewa huu utasaidia kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli na hivyo kuongeza tija kiuchumi kwa taifa kuanzia ngazi ya mwananchi mmoja mmoja.
“Moja ya majukumu ya PURA kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ni kuhakikisha inasimamia ushirikishwaji wa wazawa kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli, hivyo maonesho haya ni moja ya njia za kuwafikia wananchi na kuwapa uelewa wa namna bora ya kuwa sehemu ya shughuli hizo,” alifafanua.
Bw. Mollel aliongeza kuwa Watanzania wanaweza kushiriki kwenye shughuli hizi kwa kupata nafasi za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kuuza bidhaa na kutoa huduma kwa kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na kujengewa uwezo kutumia fursa zinazotokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Natoa wito kwa Watanzania wote watakaoweza kufika kwenye maonesho haya kutembelea banda la PURA ili kufahamu fursa zinazopatikana kwenye miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa nchini pamoja na namna bora ya kupata fursa husika,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mjiolojia Faustine Matiku amesema tofauti na kutoa uelewa wa masuala ya fursa na ushirikishwaji wa wazawa kwenye sekta, watakaotembelea banda la PURA watapata fursa ya kujifunza kuhusu masuala ya mnyororo wa thamani katika sekta ya mafuta na gesi, utafiti na uzalishaji unaoendelea kwenye vitalu mbalimbali nchini, hali za leseni za utafutaji, mradi wa usindikaji gesi asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG) na masuala mengine ya kiufundi.