……………………………………………………………
Mara baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Geita, kikosi cha KMC FC kesho kitaanza mazoezi kujiandaa na mchezo wa lili kuu ya NBC soka Tanzania bara pamoja na ile ya michuano ya kombe la Azam Sporti Federation CUP ASFC.
KMC FC imetoa mapumziko ya siku moja kwa wachezaji wake ikiwa ni baada ya kumalizika kwa mchezo wa jana dhidi ya Geita na kuibuka na ushindi wa magoli mawili kwa sifuri ambayo yalifungwa na wachezaji Matheo Anton pamoja na Abdulrazack Hamza.
KMC FC itakutana na Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa mzunguko wa nane wa Ligi kuu ya NBC Disemba 18 mwaka huu katika uwanja wa Jamuhuri Mkoani Morogoro ambapo malengo yakiwa ni kuhakikisha kwamba inakwenda kufanya vizuri licha ya kuwa katika mchezo huo itacheza ugenini.
Aidha kwaupande wa mchezo wa michuano ya kombe la ASFC ,KMC imepangwa kucheza dhidi ya Majimaji ya Songea mchezo ambao utachezwa katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam ambapo kwa upande wa tarehe bado haijawekwa wazi.
Katika maandalizi hayo ambayo yataenda kuanza kesho, kikosi hicho chini ya kocha Mkuu John Simkoko na wasaidizi wake Habibu Kondo pamoja na Hamadi Ally kinajipanga kuhakikisha kwamba kinafanya vizuri katika michezo hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya michuano ya kombe la ASFC dhidi ya Majimaji ya Mkoani Songea pamoja na Ligi kuu.
Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni kwa sasa imekuwa na muendelezo mzuri katika michezo yake tangu kuanza kwa mchezo wa mzunguko wa sita ambapo imeshinda michezo miwili na kutoka sare katika mchezo mmoja na hivyo kukusanya jumla ya pointi saba na kupanda kutoka kwenye nafasi ya 15 hadi kufika kwenye nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi kuu ya NBC.
Muendelezo wa matokeo hayo unatokana na Timu kuendelea kutafuta matokeo mazuri katika michezo 22 iliyosalia hivi sasa kabla ya kumalizika mwa msimu wa Ligi kuu ya NBC 2021/2022 na hivyo kufikia malengo ambayo Timu imejiwekea mwaka huu ya kumaliza katika nafasi Nne za juu.