Naibu Waziri waArdhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozwa na Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) Donald Rweramila kuelekea kukagua mashine za uchapishaji za chuo hicho wakati wa ziara yake chuoni hapo
Naibu Waziri waArdhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na uongozi wa Chuo cha Ardhi Tabora wakati wa ziara yake mkoani Tabora jana. Kushoto ni Mkuu wa Chuo Donald Rweramila
Wajumbe wa menijementi ya Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake kati
Naibu Waziri waArdhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji Chuo cha Ardhi Tabora Playgod Lema (Kushoto) alipofanya ziara katika chuo hicho
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia baadhi ya machapisho yaliyofanywa na Chuo cha Ardhi Tabora kupitia idara yake ya Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji Chuo cha Ardhi Tabora alipofanya ziara katika chuo hicho jana. Nyuma yake ni Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora Donald Rweramila (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
………………………………………………….
Na Munir Shemweta, WANMM TABORA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekitaka Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) kuitangaza idara yake ya uchapishaji ili iweze kufahamika na kutumika kwa shughuli za uchapishaji yakiwemo machapisho ya serikali.
Dkt Mabula alisema hayo tarehe 5 Novemba 2021 alipofanya ziara katika chuo cha ARITA kukagua utendaji kazi akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Tabora.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo, Chuo cha Ardhi Tabora kinatakiwa kijitangaza hasa idara yake ya uchapishaji kwa kuwa kazi za idara hiyo zinaweza kukiingizia mapato chuo itakayoweza kutumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya chuo.
“Tungetumia sehemu ya printing ya chuo hiki tungweza kupata fedha nyingi hivyo tunatakiwa tuitangaze idara hii ya uchapishaji kwa kuwa Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali haiwezi kufanya kazi zote na pale ofisi hiyo itakapozidiwa basi chuo hicho kifanye kazi hiyo”. Alisema Dkt Mabula
Mkuu wa idara ya Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji wa Chuo cha Ardhi Tabora Praygod Lema alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa, idara hiyo pamoja na kufanya kazi kubwa ya uchapishaji baadhi ya nyaraka za Wizara ya Ardhi na zile za halmadhauri ya jiji la Dodoma bado ina changamoto ya mashine ya uchapishaji kutokana na zilizopo sasa kutoendana na kasi ya mahitaji ambapo aliomba idara hiyo kupatiwa mashine nyingine ya kisasa.
.
“Pamoja na changamoto mlizokuwa nazo kuna haja ya kufanya matangazo na mnaweza kutumia hata vyombo vya habari ili muweze kupata kazi na kuingiza fedha maana bila ya hivyo mtaendelea kuwa na changamoto za kifedha ” alisema Dkt Mabula.
Hata hivyo, Dkt Mabula alikipongeza Chuo cha ARITA kwa kazi nzuri pamoja na changamoto inazozikabili katika utendaji kazi wake na kuutaka uongozi wa chuo kufuatilia maombi mbalimbali inayoyapeleka Wizarani kwa ajili ya kusaidiwa.
Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Donald Rweramila alisema, pamoja na chuo cha ARITA kufanya kazi ya uchapishaji lakini hakina Maabara ya Fani ya Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji kwa ajili ya mafunzo ya vitendo jambo alilolieleza kuwa linawafanya wanafunzi kutumika zaidi uandani.
Akigeukia zoezi la urasimishaji makazi holela ambapo Chuo hicho kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo Donald Rweramila kimepatiwa Milioni 644.5, Dkt Mabula alikitaka chuo cha ARITA kushirikisha wadau kabla ya kuanza kazi hiyo kwa kufanya mikutano ili kujenga ufahamu na kubainisha kuwa, mazoezi mengi ya urasimishaji makazi holela yanakwama kutokana na kutoshirikisha wadau.
“Nitarajia mtafanya mikutano na wadau na mazoezi mengi ya urasikishaji makazi holela yanakwama kutokana na kutoshirikisha wananchi na usiposhirikisha na kujua changamoto hamuwezi kufanikiwa”. alisema Dkt Mabula
Chuo cha Ardhi Tabora kinatarajia kufanya mazoezi ya urasimishaji makazi holela katika maeneo ya Tabora, Geita na Kasulu mjini mkoani Kigoma na tayari chuo hicho kimeshatambua viwanja 27,000.