Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa vyuo vya Elimu ya Juu (TAHLISO) Hija Mirambo akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tamasha la wana vyuo litalofanyika Dar es Salaam.
****************
*Hamonize kupamba tamasha hilo
JUMUIYA ya Wanafunzi Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania ambayo inajumuisha vyuo vya kati (TAHLISO) imeandaa tamasha maalum kwa wanavyuo litakalofanyika Disemba 10 mwaka huu katika viwanja vya Kijitonyama, Posta jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza, kuwakutanisha, kubadilishana mawazo ya kitaaluma na michezo na kupata burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali kutoka wa hapa nchini akiwemo Harmonize ‘Konde Boy,’ Stamina na Linah Sanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Hija Mirambo amesema kuwa tamasha hilo ni maalum kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na kati kutoka vyuo mbalimbali vya Mkoa wa Dar es Salaam ambao watakutana na kubadilishana mawazo na uzoefu na kupata burudani.
‘’Jana tulikuwa na mkutano mkuu uliowakutanisha marais wa vyuo vyote nchini na kati ya vitu tulivyojadili ni katiba mpya ambayo itaongoza jumuiya yetu na moja kati ya jambo lililozungumzwa ni kuzuia watu au taasisi kufanya matamasha kwa jina la wananfunzi bila idhini ya jumuiya ya wananfunzi wenyewe yaani TAHLISO, kwa hili tutakuwa wakali kwa sababu watu wanaharibu taswira ya wanafunzi kwa kuandaa matamasha ya ajabu ambayo hayabebi hadhi ya wanafunzi Tanzania.’’ Amesema.
Amesema Jumuiya hiyo ambayo mlezi wake ni Rais wa JamhurI ya Muungano wa Tanzania inajumuisha vyuo vikuu na kati Tanzania kote itaendelea kuwahudumia wanafunzi wa chuo kwa kuhakikisha wanapata huduma bora ikiwemo mikopo na elimu wawapo vyuoni.
Kwa upande wake Kamishina wa Michezo na Burudani wa vyuo vikuu na kati Muba Saedo amesema wamekuwa na utamaduni wa kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwenye taasisi hizo za kisomi.
‘’gharama za kiingilio kwa tamasha hili ni shilingi elfu kumi tuu, kutakuwa na huduma za vyakula na vinywaji pia… tunawaomba wanavyuo wajitokeze kwa wingi zaidi katika tamasha hili ambalo limepewa baraka la wakuu wa Wilaya, vijana na wanafunzi.’’ Amesema.
Tamasha hilo litasindikizwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Harmonize, Linah Sanga, Country Boy, Young Lunya, Stamina, Moni Centrozone na Raptcha.