Mkuu wa wilaya ya Arumeru , Richard Ruyango akimkabithi kitabu ,mwandishi wa kitabu hicho, Mwalimu David Inzofu ishara ya uzinduzi wa kitabu hicho .(Happy Lazaro)
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya kusambaza na kuuza vitabu ya Kase Stores Ltd ya jijini Arusha,Fanuel Kagengere akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa kitabu hicho jijini Arusha .(Happy Lazaro)
Mwandishi wa kitabu cha East Africa Basic Mathematics for Upper Primary Classes ,Mwalimu David Inzofu akizungumza katika uzinduzi wa kitabu hicho jijini Arusha
*******************************
Happy Lazaro,Arusha
Arusha.Mkuu wa wilaya ya Arumeru ,Richard Ruyango amesema Tanzania bado tunakabiliwa na changamoto ya waandishi wa vitabu kwani waliopo ni wachache sana hivyo kuwataka walimu nchini nje na taaluma yao ya kufundisha wajikite katika uandishi wa vitabu .
Ameyasema hayo wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha hisabati kilichoandikwa na mwandishi wa vitabu ,Mwalimu David Inzofu ambacho kitakuwa kinatumika katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema kuwa, kwa hapa nchini bado tuna waandishi wachache wa vitabu hasa katika somo la hisabati kwani hata waliopo hawatoshelezi kulingana na mahitaji yaliyopo ,hivyo kuwataka walimu na wadau kujikita katika uandishi wa vitabu ili tuweze kutumia vitu vya kwetu zaidi.
Amesema kuwa,uandishi wa kitabu hicho umezingatia maudhui yote ya somo la hisabati ambalo litamwezesha mwanafunzi kuweza kujisomea na kuelewa kwa urahisi zaidi na kuweza kuliona somo la hisabati ni rahisi na sio gumu kama wengi wanavyodhani.
“Kilichofanywa na mwalimu huyu ni Jambo zuri Sana na amekuwa na udhubutu wa hali ya juu hasa katika somo la hisabati ,kama serikali tupo tayari kumuunga mkono katika kuendeleza juhudi zake kwa lengo la kuinua kiwango cha ufaulu mashuleni hasa katika somo la hisabati.”amesema .
Naye Mwandishi wa kitabu hicho , chenye jina la East Africa Basic Mathematics for Upper Primary Classes ,Mwalimu David Inzofu amesema kuwa, amefikia hatua ya kuandika kitabu hicho kwa lengo la kuwarahisishia walimu pamoja na wanafunzi katika nchi za jumuiya kuweza kusoma somo hilo la hisabati kwa urahisi zaidi na kuweza kueleweka .
David amesema kuwa, kitabu hicho kinakithi malengo yote ya mitaala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na hiyo itasaidia pia kuongeza wigo mpana kwa wanafunzi hao katika somo hilo kwani wanafunzi wa kitanzania watakuwa na uelewa mkubwa wa kuweza kushindana na wenzao wa nchi zingine .
“Naiomba serikali iweze kuruhusu kitabu hiki kitumike mashuleni kama kitabu cha kiada, pamoja na kuziomba mamlaka za elimu kutoa ushirikiano na kukitambua kitabu hiki ili kiweze kutumika mashuleni katika nchi za Jumuiya kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu hasa somo la hesabu .”amesema.
Inzofu ameongeza kuwa ,wanafunzi wengi hawapendi kusoma somo la hisabati kutokana na kuliona ni gumu ila kupitia kitabu hiki wataweza kupenda somo hilo na kutoa motisha kwa wanafunzi kuanzia darasa la tano hadi la Saba kufanya vizuri katika masomo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kase Stores Ltd inayosambaza na kuuza vitabu ,Fanuel Kagengere amesema kuwa uwepo wa kitabu hicho ambacho ni cha tofauti kutokana na kulenga utoaji wa elimu kwa nchi za jumuiya kitasaidia Sana kupanua wigo wa wanafunzi kuweza kujifunza hesabu na kuinua kiwango Cha ufaulu mashuleni.
Amesema kuwa, changamoto kubwa iliyopo ni kuwepo kwa waandishi wa vitabu wachache ambao hawakidhi soko kulingana na uhitaji uliopo na hii ni kutokana na watanzania kutokuwa na tabia ya kujisomea vitabu hali inayosababisha kutokuwepo kwa mwamko mkubwa wa waandishi hao.