NA
K-VIS BLOG/Khalfan Said, Mbeya.
IDADI ya madaktari wenye
ujuzi wa kufanya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi imepanda na
kufikia 1,323 nchi nzima, Mkurugenzi Mkuu wa, Mfuko wa
Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amesema.
Dkt. Mduma ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya siku tano yaliyoandaliwa na WCF ili
kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma za afya jinsi ya kufanya tathmini za
ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi kutoka mikoa saba ya Nyanda za Juu
Kusini ikiwemo, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Ruvuma, Njombe na Iringa.
“Tukiwa
tunaelekea mwaka wa saba tangu Mfuko uanze kutekeleza majukumu yake, ninyi
ambao mmepatiwa mafunzo hapa, mnafanya idadi ya madaktari wenye ujuzi wa kufanya
tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi kufikia 1,323 kwenye mikoa
yote Tanzania Bara.” Alisema.
Aidha Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar alisema madaktari hao walijifunza mambo mbali mbali ikiwemo sheria ya fidia, jinsi ya kuwasilisha madai kwa njia ya mtandao, kusajili
waajiri na namna wanavyoweza kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa njia
ya mtandao, namna ya kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi
na Mafao yatolewayo na Mfuko,
Kwa upande wao, washiriki
hao waliupongeza Mfuko kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wameeleza yamekuwa na
manufaa makubwa kwao.
“Nimejifunza
mambo mengi ambayo nilikuwa siyafahamu,mfano sasa nimejua ya kwamba mtu
anapokuwa amepata ajali itakayompelekea kupata ulemavu atastahili kufanyiwa
tathmini pale tu atakapofikia kiwango cha juu cha kupona yaani maximum medical improvement.”. Dkt.
Adolph Daudi Ntilagana, Hosptali ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi alisema.
Mshiriki mwingine Dkt.Pronent
Mtei kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya alisema mafunzo hayo
yamembadilisha kwani hivi sasa ameelewa kwamba Mfuko unaweza kumpatia matibabu
au fidia mfanyakazi anapoumia au kuugua kutokana na kazi.
“Nimejifunza
na kuelewa tofauti ya magonjwa yatokanayo na kazi na yale ambayo hayatokani na
kazi, hivyo itakuwa rahisi kwangu mteja anapokuja kwa changamoto ya maradhi
kuweza kumtambua kama tatizo lake lina vigezo au la kwa mujibu wa mwongozo wa
WCF.” Alisema Dkt. Mtei
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, (MZRH) Dkt. Godlove Mbwanji ambaye ndiye
aliyafunga mafunzo hayo aliwaasa madaktari na watoa huduma za afya kuzingatia
yale waliyojifunza wakati watakaporejea kwenye vituo vyao vya kazi.
“Mafunzo haya
yatatusaidia sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini kuweza kufanya tathmini sahihi
ambayo itauwezesha Mfuko kutoa fidia stahiki na kwa wakati.” Alisisitiza.
Dkt. Francis Chila (kulia) na Innocensia William wote kutoka WCF wakipitia dodoso maalum tayari kuwagawia washiriki kwa uelewa wa mafunzo