Mkuu wa Wilaya Kaliua Mkoani Tabora Paul Chacha akifungua warsha ya siku moja ya kuwajengea uwezo viongozi wa chama wilayani humo
Katibu wa Chama Cha Walimu Wilayani Kaliua, Kessy Kidifu
Baadhi ya wajumbe wa chama cha walimu wilaya ya Kaliua wakisikiliza wamaelekezo ya viongozi wao
Katibu wa chama cha walimu mkoa wa Tabora, Digna Nyaki akisitiza jambo kwa wajumbe wa chama cha walimu wilaya ya kaliua mkoani hapa
………………………………………………………………………
Na Lucas Raphael,Tabora
Chama cha cha walimu mkoani Tabora kimeshauriwa kuwa na subira wakati Taifa linaendelea kushughulikia changamoto na madai mbalimbali ya watumishi nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya Kaliua mkoani Tabora, Paul Chacha katika warsha ya siku moja ya kuwajengea uwezo viongozi wa chama wilayani humo ilifanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Kaliua.
Alisema kwamba serikali ya awamu ya sita imedhamiria kushughulikia changamoto mbalimbali na madai ya watumishi nasio walimu tu bali wafanyakazi wote nchini.
Alisema kwamba serikali imeanza kulipa madai mbalimbali ya watumishi wa kada zote wakiwemo walimu pamoja ,kupandisha na kuwapandisha madaraja watumishi wake .
Alisema kwamba walimu ni hatua na nguzo ya kwanza katika maendeleo ya taifa na kwamba serikali inatambua mchango wao na hivyo hawana budi kutembea kifua mbele.
“Upungufu wa walimu katika shule za sekondari na msingi, madai ya mishahara na yasiyokuwa ya mishahara yanaendelea kushughulikiwa katika ngazi ya kitaifa hivyo tuwe na subira na changamoto hizi hazipo kwa walimu pekee bali kwa watumishi wote nchini.’’alisema mkuu wa wilaya Chacha
“Hata hivyo, changamoto ambazo zipo ndani ya uwezo wangu kama Mkuu wa Wilaya sitasita kuzitatua ili haki ya mtumishi na raia awaye yote wa nchi hii aishie Wilayani humu ilindwe. Simu yangu iko wazi masaa 24 hivyo karibuni sana.’’ Alisisitiza.
Awali akisoma risala mbele ya Mkuu wa Wilaya , Katibu wa Chama Cha Walimu Wilayani Kaliua, Kessy Kidifu alisema chama hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa walimu, malimbikizo ya madeni yakiwemo likizo, matibabu, mapunjo ya mishahara na uhaba wa nyumba za walimu shuleni.
Alisema upungufu wa walimu katika shule za sekondari 20 zilizopo ni Walimu 256 na 1,544 wa shule za msingi ili kufikia idadi ya Walimu 3,355 wanaotakiwa wilayani Kaliua.
Aidha alisema kwamba madeni ya mishahara na yasiyokuwa ya mishahara katika shule za sekondari Wilayani Kaliua mpaka sasa ni shilingi 96,426,202.67 na shilingi 141,082,225 zinazohusu matibabu na uhamisho katika shule za msingi. Alifafanua katibu huyo
Hata hivyo Katibu wa chama cha walimu mkoa wa Tabora, Digna Nyaki alisema kuwa mkuu wa wilaya hiyo amewaachia walimu zoezi la kufanya ambalo ni kufundisha kwa bidii.
Sanjali na hilo aliwataka walimu kufaulisha kwa uhalali kupitia mitihani ya ndani na kitaifa wakati serikali ikiendela kushughulikia madai yatokanayo na utumishi wao.
Chama cha walimu nchini Tanzania (CWT) kilisajiliwa 1/11/1993 kwa namba ya usajli TU. 002 chini ya sheria ya vyama vya wafanyakazi (The Trade Unions Ordinance Camp No. 381 ya mwaka 1956 kabla ya sheria mpya ya bunge ya vyama vya wafanyakazi (The Trade Union Act No .10 ya mwaka 1998 ambapo mwaka 2000 chama hicho kilisajiliwa tena chini ya sheria hiyo na kupata namba ya usajili TU.004.
Ilielezwa kuwa malengo mahususi ya chama hicho ni kutetea haki za walimu hususani mishahara bora, miundo ya utumishi wa walimu, kuwaendeleza walimu kitaaluma na kiuchumi, kutetea na kudai miundombinu bora kazini yakiwemo makazi bora, kusuruhisha migogoro kwenye ajira zao, kuwawezesha kutoa maoni yao kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji na kuunganisha nguvu pamoja ili kudai haki zitokanazo na utekelezaji wa majukumu yao kwa umma wa Watanzania.