Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni akipokea tuzo ya mshindi wa kwanza ya uandaaji wa taarifa za hesabu chini ya viwango vya IPSAS katika kundi la vyuo vya elimu ya juu, katika hafla iliyoandaliwa na NBAA.
Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni kushoto,, akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Makamu Mkuu wa Taasisi Utawala Fedha na Mipango Dkt. Zena mabeyo, Mhasibu Mkuu wa Taasisi CPA Athuman Senzota, akifuatiwa na CPA Aisha Kapande na Juma Ali Zuberi (wahasibu waandamizi) mara baada ya kupokea tuzo ya mshindi wa kwanza ya uandaaji taarifa za hesabu chini ya viwango vya IPSAS katika kundi la vyuo vya elimu ya juu.
Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Taasisi ya Ustawi wa Jamii
………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Ustawi wa Jamii imetunukiwa tuzo ya mshindi wa kwanza ya uandaaji wa taarifa za hesabu chini ya viwango vya IPSASs, katika kundi la vyuo vya elimu ya juu nchini kwa mara ya tatu mfululizo.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika jijini Dar Es Salaam Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dkt Joyce Nyoni amesema ni furaha sana kupata tuzo hiyo kwa mwaka mwingine kwani imewafanya kubaki kwenye viwango vya ubora katika utunzaji wa hesabu.
Dkt. Joyce Nyoni ameongeza kuwa Taasisi hiyo itaendelea kuhakikisha inasimamia matumizi ya fedha za Serikali zinazotolewa hasa katika kutekelza miradi mnalimbali ya maendeleo katika Taasisi hiyo.
“Na leo hii baada ya kuongeza juhudi tumepata tuzo ya mshindi wa kwanza ya taarifa ya hesabu ya mwaka 2020 na tunajipanga kuendelea kushika nafasi hii ya kwanza bila kushuka chini’’ alisema Dkt. Joyce.
Aidha Dkt. Joyce amewapongeza watendaji na wafanyakazi wote wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa kutukeleza majukumu yao na kuwezesha kupata tuzo hiyo amnbayo imeewapa heshima na kuaminiwa na Serikali na umma kwa ujumla katika matumizi mazuri ya fedha.
“Naomba tuendelee kushirikiana kwa pamoja, tuendelee kufanya kazi kwa uweledi kwasababu tumekuwa tukifanya hivyo, ndio maana tumepata tuzo hii wote kwa pamoja. Tuzo hii ni yetu Taasisi wote kwa pamoja’’, alisema Dkt. Joyce.
Dkt. Joyce amefafanua kuwa tuzo hizo zina tija sana katika kuipa Serikali imani na Taasisi zake ili kuihakikishia fedha zinatumika vizuri na kama zililivyokusudiwa katika shughuli mbalimbali katika Taasisi mbalimbali za Serikali.
Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii CPA Athuman Senzota amesema tuzo hizo zina maana sana kwasababu zinaipa Serikali imani na na inaonesha kwamba utawala bora lazima uendane na hesabu ambazo watu wengine waweze kuzisoma na kuelewa.
Taasisi ya Ustawi wa Jamii inachukua tuzo hii kwa mara sita mfulilzo, ikiwa imeshachukua tuzo hii mara mbili katika nafasi ya mshindi wa pili, mara moja katika nafasi ya mshindi wa tatu na mara tatu katika nafasi ya mshindi wa kwanza. Kila mwaka Bodi ya Uhasibu Tanzania hutoa tuzo hizo kwa Taasisi za umma na binafsi zilizoshiriki katika kinyang’anyiro hicho.