Natumia fursa hii kuwafahamisha kuwa, tarehe 02 Desemba 2021 kulifanyika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa hapa Dar-es salaam. Kikao hicho kilikuwa na agenda mbili. Agenda ya kwanza ilikuwa ni maandalizi ya mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa na
agenda nyingine ilikuwa ni mengineyo.
Madhumuni ya kuwaiiteni ni kuwaomba muwape Watanzania taarifa za maandalizi ya mkutano huo wa wadau, ili wahusika wote wafahamu maandalizi yalipofika na wajiandae kushiriki ipasavyo. Pia kuongea mambo muhimu machache ya kujipongeza kwa kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru. Itakumbukwa kuwa, mkutano huo ulikuwa ufanyike tarehe 21, 22 na 23 Oktoba 2021, lakini ukaahirishwa kutokana na sababu za msingi. Hivyo, tumeona ni vyema kuwafahamisha wadau wote kuwa, mkutano huu bado upo na sasa umepangwa kufanyika tarehe 16 na 17 Desemba 2021 katika Jiji la Dodoma kama ilivyokuwa imapangwa awali. Aidha, mkutano huo utatanguliwa na semina ya siku moja kwa wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa ambayo itahusu historia na majukumu ya Baraza hilo, itakayofanyika tarehe 15 Desemba 2021 katika ukumbi ambao mkutano wa wadau utafanyika.
Mkutano huu ni muhimu, kwani utawezesha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kukutana na kubadilishana mawazo na uzoefu, ili kuwezesha Sheria zinazoratibu shughuli za vyama vya siasa hapa nchini kwetu kuboreshwa
kama itahitajika, pia kujadili utekelezaji wa sheria hizo sambamba na kudumisha amani, utulivu, uzalendo, maadili na umoja wa Taifa letu. Kutokana na umuhimu wa mkutano huu, tumemualika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi na kuufungua. Mkutano utajumuisha wadau mbalimbali wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, ikiwamo wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa, viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa ambayo siyo wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa, viongozi wa Dini ngazi ya Taifa, Taasisi zisizo za Kiserikali (AZAKI), Viongozi wa Serikali, Waandishi wa Habari, Taasisi za Serikali na Watu Mashuhuri. Mada tatu zitawasilishwa na wataalamu wabobezi, kisha kujadiliwa na washiriki wa mkutano. Mada zitahusu masuala ya kisheria, demokrasia, siasa, uchumi na maadili ya kitaifa, yanayohusiana na demokrasia ya vyama vingi vya siasa. Hivyo, Baraza la Vyama vya Siasa linatumia fursa hii, kushauri vyama vya siasa vyote vyenye usajili kamili, kuhudhuria mkutano huo, kwani ni fursa adhimu ya kubadilishana mawazo kuhusu mambo yanayotuhusu. Siasa ni ushawishi na ushawishi hufanikiwa kapitia njia ya mijadiliano.
Aidha, kwa kuwa mwezi huu wa Desemba 2021 tunasherehekea miaka 60 ya uhuru wa nchi yetu, tumeona ni vyema kuongea kuhusu suala hilo pia. Tuanze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na kujipongeza Watanzania wote kwa uhuru wa nchi yetu kutimia miaka 60 na hatua kubwa ya kimaendeleo tuyofikia katika muda huo. Pamoja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii tuliyopata katika miaka 60 ya uhuru, nchi yetu imeendelea sana katika masuala ya demokrasia na siasa, na ni mojawapo wa mifano ya kuigwa dunia. Mojawapo ya masuala makubwa tuliyofanikiwa sana katika demokrasia na siasa, ni kuendesha mfumo wa demokrasia uliokuwapo na uliuopo sasa, katika hali ya amani, utulivu, uzalendo, kimaadili na umoja wa kitaifa, huku tukilinda uhuru wetu. Haya ni mafanikio makubwa ambayo nchi nyingi zimeshindwa kuyapata kama ilivyo sisi. Hivyo, tuna haki ya kujivunia na kuyadumisha. Changamoto zipo, lakini ni zile zinazozungumzika na kutalitulika. Tanzania ni nchi huru na tumefanikiwa kulinda uhuru wetu kama tulivyoeleza hapo awali. Hivyo, tunawaasa wananchi wote ikiwamo vyama vya siasa, tuendelee kulinda uhuru wetu. Tanzania huru ina Katiba nzuri inayotoa haki za kidemokrasia na kisiasa kwa kila mtu, ambapo vyama vya siasa vinaandikishwa
na kufanya shughuli zake kwa uhuru unaohitajika. Kuna vyombo vya haki na kidemokrasia kama Bunge, Mahakama na vyombo vya habari, ambavyo vipo huru na vinafanya kazi kwa weledi na haviingiliwi na mtu au taasisi yoyote. Hivyo, tunaomba jumuiya ya kimataifa, ishirikiane nasi kudumisha uhuru na utashi wetu, na asitokee mtu au taasisi au nchi ya kutupangia kitu cha kufanya kwani kila nchi ina mambo yake. Katika nchi yetu pia kuna Baraza la Vyama vya Siasa ambalo linakutanisha viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa vyote vyenye usajili kamili. Katika Baraza la Vyama vya Siasa tunajadili masuala mbalimbali yanayotuhusu vyama vya siasa na kama kuna changamoto tunazijadili na wahusika ili kupata ufumbuzi. Hivyo, Baraza la vyama vya siasa ni sehemu nzuri na muafaka kwa vyama vya siasa kubadilishana mawazo na kujadili changamoto zinazojitokeza, kuliko kwenda kuongelea changamoto hizo katika vyombo vya habari au sehemu nyingine ambazo muhusika hana nafasi ya kuzijadili ili kupata ufumbuzi wake. Hivyo, tunatumia fursa hii pia kuishukuru Serikali kwa kufanya Baraza la Vyama vya Siasa kuwa ni chombo cha kisheria, ambacho kipo kwa maslahi ya taifa letu la Tanzania, ikiwamo kudumisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa tulionao. Tunamalizia kwa kuwapongeza viongozi wa nchi yetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa jinsi wanavyoongoza vyema nchi yetu na kutupatia mafanikio zaidi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, kama tulivyoeleza. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape afya njema, ili waendelee kuchapa kazi, na kazi iendelee. Namalizia kwa kuwasalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzani