…………………………………………………
Na Asila Twaha, OR – TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya) Dkt. Grace Magembe amewataka wataalam wa Afya wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuepuka migogoro isiyoleta manufaa katika kusimamia ujenzi wa miradi ya ujenzi wa EMD na ICU.
Akizungumza hayo Desemba 03, 2021 Jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi Cha kuwajengea uwezo Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri, Waganga Wafawidhi na Wahandasi katika kusimamia miradi ya ujenzi wa majengo ya dharura (EMD) na ICU Dkt.Grace amesema siku walizokuwepo katika kikao hicho wanaporudi kwenye vituo vyao vya kazi waende wakashirikiane kwa kusimamia na kutekeleza miradi ya ujenzi wa EMD na ICU kwa ubora na wakati lengo likiwa wananchi waweze kupata huduma kwa haraka.
TAMISEMI imetengewa shilingi bilioni 493.9 sawa na asilimia 38 na fedha zote hizi ni kwasababu ya sekta zilizopata athari za kiuchumi kutokana na ugonjwa wa COVID-19.
Aidha, amesema fedha zilizotolewa shilingi bilioni 236 kwa upande wa afya ni kutekeleza miradi inayolenga kujikinga ugonjwa wa COVID -19 ikiwemo miradi ya ujenzi wa majengo ya dharura na ICU.
Akiendelea kufafanua Dkt. Grace amesema kuwa, fedha hizo zimeelekezwa kutekeleza afua mbalimbali za kukabiliana na athari za COVID -19 ikiwemo ujenzi wa ICU 26, EMD 80, ununuzi wa magari ya kubebea wagonjwa(ambulances) 195, ujenzi wa mitambo mikubwa 6 ya kuzalisha oksijeni ambapo itakuwa na uwezo wa kuzalisha mitungi 200 kwa masaa 24 na ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya kuimarisha huduma katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
“Natoa wito twendeni tukasimamie, wananchi wanataka huduma sio mivutano asiye taka kufuata utaratibu kwa wakati hatua zitachukuliwa na ujenzi wa ICU na EMD unatakiwa usimamiwe kwa umakini ukikosea ujenzi maanayake hata kutoa huduma utakosea” amesisitiza Dkt. Grace
Mganga Mkuu wa Mkoa Mara Dkt. Juma Mfanga ameishukuru Serikali kwa kuleta fedha za miradi ya ujenzi wa EMD na ICU na kuihakikishia wanaenda kushirikiana kwa ukaribu na watendaji wote wakiwemo na wahandisi ili kazi hiyo ifanyike kwa waledi, ubora na kukamilika kwa wakati.