Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akizungumza wakati alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Irkujit wilayani Simanjiro mkoani Manyara kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo ya Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akizungumza na wananchi wakati alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa josho la kuogeshea mifugo katika Kijiji cha Irkujit wilayani Simanjiro mkoani Manyara kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo ya Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akiwa na kikundi kilichonufaika na mradi wa ujenzi wa ufugaji wa mbuzi Jitegemee wilayani Simanjiro mkoani Manyara kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo ya Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Sehemu ya wanachi wa Kijiji cha Irkujit wilayani Simanjiro mkoani Manyara wakiwa katika josho la kunyweshea mifugo lililojengwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo ya Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
**************************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amesema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi wilayanj Simanjiro mkoani Manyara.
Jafo ametoa kauli hiyo leo Desemba 4, 2021 alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo ya kukagua miradi hiyo inayotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia fedha za Mfuko wa Mazingira Duniani (Global Environmental Facility) chini ya Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia (EBARR).
Katika ziara hiyo ndani ya wilaya ya Simanjiro, Jafo alitembelea mradi wa ufugaji wa mbuzi, mradi wa birika la kunyweshea ng’ombe, mradi wa josho la kuogeshea ng’ombe, mradi wa kuku chotara pamoja na mradi wa kiwanda cha ngozi.
Akiendelea kuzungumza alioneshwa kufurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo iliyo zingatia mahitaji halisi ya jamii sambamba na thamani ya fedha huku akiagiza miradi hiyo yote iwe imekamilika na kuzinduliwa ndani ya mwezi mmoja ujao.
Miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi imekuwa ikitekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuibuliwa na wananchi katika maeneo husika na imekuwa ni msaada mkubwa sana katika jamii.
Aidha, miradi hiyo inatekelezwa katika halmashauri za wilaya tano za Simanjiro, Kishapu, Mpwapwa, Mvomero na Wilaya ya Kaskazini A Unguja. Miradi hiyo ya kuhimili mabadiliko ya Tabia nchi inagharimu dola za Kimarekani milioni 7.5 sawa na wastani wa Sh. bilioni 17.4 kwa wilaya zote tano.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt. Suleiman Serera aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuja na mradi huo wilayani humo na kusema imekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa siri ya mafanikio katika kutekeleza miradi hiyo ni uwepo wa watumishi wanaojitambua katika kuisimamia hali inayosaidia uongozi kuwasimamia vizuri.