……………………………………………………………..
Na Silvia Mchuruza,Muleba.
Katika kutunza na kulinda rasilimali za nchi, kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila inawashikilia watu 28 wakazi wa Kijiji cha Kyota kata ya Kimwani waliokutwa wakijihusisha na uvuvi haramu kwa kutumia makokoro saba na mitumbwi saba yenye jumla ya thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 12.
Akizungumza mara baada ya kuwakamata watuhumiwa hao, Mhe. Nguvila amesema kuwa watu hao walikamatwa na wananchi usiku wa kuamkia tarehe 02 Desemba 2021katika kitongoji cha Kabwinyora, kijiji cha Kihunge, kata ya Rulanda wakiwa ndaniya ziwa Victoria.
“Nina fahamu haya makokoro na maboti hawa sio matajiri wako matajiri waliowatuma na bahati nzuri baadhi yao majina tunayo wote hawa tunaendelea na uchunguzi tukithibitisha tuawamata na kuwapeleka mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine”, ameeleza Mhe. Nguvila.
Ameendelea kueleza kuwa Wilaya inaendelea kufuatilia mtandao wa watu hawa wanaowafadhili na kuwatumia wavuvi wadogo kufanya uvuvi haramu, kwani wanaamini hawako peke yao, wakiwabaini wote wanaojihusisha hatua za kisheria zitachukuliwa lengo ni kulinda rasilimali za ziwa Victoria.
Aidha, Mhe. Nguvila amewashukuru wananchi waliojitokeza kushiriki kwa hiari yao kuwakamata watu hao wakiwa ndani ya ziwa wakati wanavua samaki wachanga kwa kutumia makokoro . Pia amewataka wakazi wa mwambao wa ziwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi ili kudhibiti uvuvi haramu.
Awali Kaimu Afisa Uvuvi Wilaya ya Muleba Bwana Johaiveni Kyaruzi amesema kuwa eneo la Kabwiyorwa kwa mujibu wa sheria ni eneo la hifadhi ya mazalia ya samaki kutokana na kuwa kuna mkondo wa maji hivyo endapo watu wakiendelea kuvua samaki kwa makokoro yaliyo kinyume cha sheria mazalia ya samaki yataisha.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Rulanda Mhe. Evart Ernest Tiletwa amesema kuwa wananchi wa kitongoji hicho kwa hiari yao waliamua kuweka doria wenyewe ili kudhibiti uvuvi haramu usiokubarika kisheria hii ni kutokana na kata hiyo kutokuwa na Afisa Uvuvi pamoja na vitendea kazi ikiwemo boti kwa ajili ya doria.
Nao baadhi ya wananchi walioshiriki zoezi la ukamataji wa makokoro na watu hao, Bwana
Mbaraka Yunusu amesema kuwa pamekuwa na tabia ya watu kutoka kata za jirani kwenda katika eneo hilo kuvua samaki kwa njia zilizo kinyume cha sheria hivyo kupelekea kuharibu mazalia ya samaki hivyo wamehaidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa wilaya ili kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu ndani ya Wilaya ya Muleba.