Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike, akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mwongozo wa matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi mkoani humu
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Lishe, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, Mwita Waibe,akisoma mwongozo wa matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwa maofisa elimu sekondari,wakuu wa shule na wadau wa elimu mkoani Mwanza (hawapo pichani).
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Lishe, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, Mwita Waibe (mbele kulia) akisistiza jambo kwa washiriki wa kikao cha tathmini ya mwongozo wa matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi (hawapo pichani).
Washiriki wa kioa cha tathmini ya mwongozo wa matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virubitushi ( pichani) wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Lishe, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, Mwita Waibe (mbele kulia).Picha na Baltazar Mashaka
………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
MATUMIZI ya vyakula viliovyoongezwa virutubishi yatasaidia wanafunzi kuepuka tatizo la udumavu,upungufu wa damu na madini kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 na wanawake wa zaidi ya miaka 15 hadi 49.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza,Ngusa Samike,wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mwongozo wa matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi mkoani humu.
Alisema Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa yenye tatizo la utapiamlo ambapo utafiti uliofanywa na TNNS mwaka 2018 ulionyesha kiwango cha udumavu ni asilimia 29.3,ili kupunguza tatizo hilo inahitajika mikakati ya uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula vitakavyotumika shuleni na kwenye jamii.
Ngusa alisema,serikali inafanya jitihada za kuzingatia lishe kwenye shule za sekondari 303 zilizopo mkoani Mwanza,ni shule 50 tu za bweni sawa na asilimia 16 zinazotumia vyakula vilivyoongezwa virutubishi,huku shule za msingi 1,091 zikiwemo za bweni 158 na za kutwa 861,kati ya shule hizo zote 158 sawa na asilimia 15.5 ndizo zinatumia vyakula hivyo.
Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri kutenga bajeti ya lishe pia maofisa elimu na wakuu wa shule wahakikishe wanafunzi wanatumia unga wa mahindi ulioongezwa virutubishi aina ya foliki asidi,zinki,madini chuma,madini ya zinki kwenye ngano,vitamini ‘A’ katika mafuta ya kula, vitamini B12 na madini joto kwenye chumvi ili wanafunzi kupata wapate lishe bora.
“Utapiamlo upo kwenye nchi nyingi duniani,ni mkubwa zaidi kwenye nchi masikini na zinazoendelea ikiwemo Tanzania.Tuhakikishe shule zote zinatekeleza hili,jitihada gani zifanyike maana watoto wana feli, inawezekana ni udumavu wa akili na tutapita kila shule kukagua kuona maelekezo ya serikali kama yanazingatiwa,”alisema Ngusa.
Alifafanua kuwa makundi yanayoathirika zaidi kutokana na changamoto hiyo, ni watoto wa umri chini ya miaka 5 na vijana wa rika balehe na kusababisha kupata upungufu wa damu na uelewa duni wa mtoto kujifunza darasani, udumavu wa kimwili na kiakili pamoja na athari za kukua kwa mtoto.
“Ni dhahiri Mkoa wa Mwanza una changamoto ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 wana tatizo la upungufu wa damu,takwimu zinaonyesha ni asilimia 46 ya watoto hao na wanawake wenye umri wa miaka 15-49 ni asilimia 52,wakitumia vyakula vilivyoongezwa virutubisha kama unga wa mahindi ulioongezwa madini chuma utasaidia kuondoa tatizo hilo,”alisema Ngusa.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Lishe, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, Mwita Waibe,serikali inaandaa mikakati ya kusimamia suala la udumavu ili kuupunguza na haitarajii watoto watumie chumvi,unga na mafuta yasiyorutubishwa,pia chakula chenye virutubishi kisitumike shuleni tu bali na kwenye jamii.
“Tatizo ni kubwa nchini,tuna asilimia 32 ya watoto wamedumaa hawafundishiki, mtaji huu wa rasilimali watu bado hatujajiandaa kukuza uchumi hivyo shule zianze kutumia vyakula vilivyoongezwa virutubisho tuhakikishe tunasimamia ubora wa vyakula na uhifadhi, tusiache kuzikagua shule binafsi pia tutashirikisha wasindikaji wa vyakula waongeze virutubisho wakizingatia sheri na kanuni,”alisema
Waibe alisistiza vyakula viongezwe virutubisho kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi ili kukabiliana na udumavu, upungufu wa damu, vitamini na madini, bodi za shule zijielekeze kwenye mikataba ya lishe na shule zote watoto wale vyakula vyenye virutubisho (unga wa mahindi, ngano,mafuta na chumvi).
Aidha Mkuu wa Shule ya Sekondari Sengerema, Zakaria Kahema, alisema baada ya mwongozo kutolewa watakwenda kuutekeleza na kuhakikisha unakuwa na tija kwa watoto kula chakula chenye ubora unaokidhi viwango.
Mkurugenzi wa Nyota Rays Food Proccesing & Packaging (NFPP) Ltd, Moses Buhilya,alisema serikali kutoa chakula shuleni imepiga hatua kubwa ya kupongezwa,kwa wasindikaji ni jambo la kujivunia na watahakikisha wanatengeneza na kuzalisha chakula chenye ubora kwa kuzingatia viwango kwa bei inayohimilika kwenye soko kwani virutubisho watapewa bure.