…………………………………………………………
Nà Silvia Mchuruza,Muleba,Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila ameagiza kusimama kwa shughuli za kuendeleza eneo linalomilikiwa na Taasisi ya Biirabo Rural Transformation Scheme Trust Fund (RTSTF) lenye ukubwa wa hekta 35.4 ambalo lina mgogoro na wananchi wa Kijiji cha Kihumulo, Kata ya Biirabo, Wilaya ya Muleba ili kujiridhisha endapo taratibu zote za kisheria kama zilifuatwa wakati wa kumilikishwa eneo hilo.
Agizo hilo amelitoa baada ya kubaini kuwa hakuna nyaraka zinazoonesha kuwa wamiliki wa eneo hilo walifuata taratibu za kisheria kwani hakuna mihtasari yoyote ya ngazi za kijiji iliyoridhia kuwagawia eneo hilo.
“Mgogoro huu umedumu kwa muda mrefu, hakuna mihtasari ya Kijiji inayoonesha kuwa taasisi hii mlipewa eneo hili kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za ugawaji na umiliki wa ardhi, hivyo naagiza kusimama kwa shughuli zote za uwekezaji na uendelezaji wa eneo hili, mpaka pale tutakapojiridhisha kuwa mlimilikishwa kwa kufuata taratibu,” ameeleza Mhe. Nguvila
Aidha amewaeleza wananchi kuwa ameletwa kuwatumikia wananchi na yupo kwaajili ya kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi wote wa Wilaya ya Muleba, hivyo atahakikisha anatatua kero na migogoro inayowasilishwa kwake kwani moja ya majukumu ya Serikali ni kuwahudumia na kutatua kero za wananchi.
Ameendelea kuwaonya viongozi wa Serikali za Vijiji katika maeneo yote ya Wilaya ya Muleba ambao wamekuwa wakigawa maeneo ya Vijiji pasipo kufuata utaratibu huku akiwataka watu na Taasisi zinazotaka kumiliki ardhi kufuata utaratibu kama Sheria ya Umiliki wa Ardhi inavyoelekeza.
Katika ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mwanasheria wa Halmashauri na Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.