Mkuu wa Mkoa wa Joseph Mkirikiti (kulia) akiongea na viongozi na watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa madarasa katika shule ya sekondari Miangalua
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Miangalua iliyopo Laela ambapo amewasihi kusoma kwa bidii kwani serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Lightness Msemo (kulia) jana wakati aipokagua ujenzi wa madarasa sita shule ya sekondari Uchile iliyopo Laela.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Lightiness Msemo akiongea kwenye mkutano wa hadhara wa utoaji elimu ya UVIKO-19 jana katika eneo la Laela wilaya ya Sumbawanga.
………………………………………………………………
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Lightness Msemo amesema kazi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 87 chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 yatakamilika kwa ubora na wakati .
Ametoa kauli hiyo wakati akitoa taarifa ya miradi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliyefanya ziara ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo kwenye wilaya ya Sumbawanga.
“Tuna mipakani ya kuendelea na kazi usiku na mchana ambapo timu zangu za usimamizi zipo kwenye maeneo ya mradi. Tumekubaliana kuwa ifikapo tarehe 10 Desemba mwaka huu tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa madarasa yote 87 kwenye shule za sekondari na vyumba 17 vya vituo shikizi vya shule za msingi” alisema Msemo.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa tayari vifaa vyote vya madukani vinavyohitajika kwa kazi ya ujenzi wa madarasa hayo vipo na kazi kubwa inayofanyika ni kuongeza ufuatiliaji na usimamizi wa mafundi ujenzi ili kazi iwe bora na kukamilika kwa wakati.
Kwa mujibu wa mgao wa fedha Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilipokea shilingi 1,740,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 87 vya madarasa na shilingi 340,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 17 katika vituo shikizi vya shule ya msingi .
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alimtaka Mkurugenzi na wataalam wote kuongeza kasi ya usimamizi wa miradi hiyo kwani katika baadhi ya shule alibaini kuwa baadhi ya madarasa ujenzi wake bado upo kwenye hatua ya msingi.
Mkirikiti alionya kuwa halmashauri hiyo haipaswi kuwa ya wa mwisho kukamilisha miradi hiyo kwani fedha walipatiwa mapema mwezi Octoba mwaka huu kama zilivyo halmashauri zingine na kuongeza kuwa hatokuwa tayari kuona miradi hiyo ikikwama.
“Rais Samia Suluhu Hassan anataka nchi iondokane na tatizo la upungufu wa madarasa na madawati ndio maana ameleta fedha hizi kote ili tujenge na kuwezesha wanafunzi kusoma kwenye mazingira mazuri. Kazi yetu kama viongozi mkiwemo ninyi madiwani ni kufanya usimamizi na ufuatiliaji ili matumizi ya fedha hizo yalete tija kwa wananchi” alisema Mkirikiti.
Katika hatua nyingine Mkirikiti alitoa onyo kwa baadhi ya madiwani ambao wameonesha kutounga mkono jitihada za serikali kwa kuwazuia wananchi kujitokeza kwenda kuchangia nguvu kazi kwenye miradi ya maendeleo.
Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa Mkoa alitoa agizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kamati za ujenzi wa miradi hiyo kama ilivyoagizwa na serikali kupitia Mwongozo wa utekelezaji uliotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI uzingatiwe kwa wananchi kushirikishwa.
“Nataka kuona kuona kamati za ujenzi zikitumika ambapo wananchi ni budi wakashirikishwa. Aidha nataka kila mradi uwe na mihutasari ya vikao kuonesha kazi zinavyofanyika eneo la mradi yote” alisisitiza Mkirikiti.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alikagua ujenzi wa madarasa kwenye shule za sekondari za Miangalua, Uchile, Lusaka, Kwela, na Mpui zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.