Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na wahitimu kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kijitonyama Dar Es Salaam wakati wa Mahafali ya 45 ya Taasisi hiyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis akitoa cheti kwa mmoja wa wahitimu kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kijitonyama Dar Es Salaam wakati wa Mahafali ya 45 ya Taasisi hiyo.
Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Taasisi ya wa Jamii
……………………………………………………
Na Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amemuagiza Kamishna wa Ustawi wa Jamii kushirikiana na Menejimenti ya Taasisi hiyo kuainisha maeneo ya ushirikiano na kupanga mikakati ya pamoja ili kuwatumia wahitimu katika utoaji wa huduma za jamii, tafiti na ushauri wa kitaalamu.
Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema hayo leo Desemba 3, 2021 katika mahafali ya 45 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika mkoani Dar Es Salaam.
Amesema hatua hiyo ni kubwa katika kuimarisha uwezo wa Taasisi ambayo itawezesha kutoa wanafunzi waliobobea katika fani mbalimbali.
“Pia nimefurahishwa na jinsi mlivyoweka mkazo kwenye mafunzo ya vitendo ili kumpa mwanafunzi uzoefu na ujuzi wa ziada katika fani anayosomea. Hatua hii itapunguza ama kuondoa kabisa pengo lililopo kati ya mahitaji ya soko la ajira na uwezo wa wahitimu wetu. Alisema Naibu Waziri Mwanaidi.
“Wizara utaendelea kutoa huduma bora kwa makundi maalum nchini kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii. Hivyo basi, naagiza Kamishna ushirikiane na Menejimenti ya Taasisi hii kupanga mikakati, na nitaomba mikakati hiyo ofisini kwangu mapema,” alisisitiza Naibu Waziri Mwanaidi.
Aidha Naibu Waziri Mwanaidi amewataka wahitimu hao kusimamia misingi na maadili ya taaluma mbalimbali walizojifunza kwenye Taasisi hiyo, pamoja na kuweka uzalendo na upendo kwa nchi yao.
Pia ameipongeza Menejimenti ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia hasa kusomesha wahadhiri kwenye ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PHD).
Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara ya Maendeleo ya Jamii, Patrick Golwike amesema Wizara inaisimamia Taasisi hiyo kuweka mkazo mkubwa katika kuzalisha wanafunzi wenye umahiri na ujuzi unaotakiwa kwenye soko la ajira.
” Wizara inasimamia Taasisi katika utekelezaji wa masuala mbalimbali na imefanikisha kuanzisha kitengo cha ubunifu na mafunzo ya uanagenzi ili kuwawezesha wahitimu wetu kupata ujuzi unaohitajika kwenye soko,” alisema Golwike
Awali Mkuu wa Taasisi hiyo, Dkt. Joyce Nyoni amesema kwa mwaka wa masomo 2020/2021 katika mahafali hayo wahitimu 1,271 sawa na asilimia 68 ni wanawake na 596 ni wanaume, sawa na asilimia 32.
Hata hivyo amesema Taasisi inajivunia mafanikio iliyoyapata ikiwa ni pamoja na kuongeza udahili kutoka wanafunzi 3,159 kwa mwaka wa masomo 2020/21 hadi 5,122 kwa mwaka wa masomo 2021/22.
“Pia imeendelea kuwasomesha walimu pamoja na wafanyakazi katika ngazi mbalimbali ili kukidhi mahitaji yetu na kuendana na kasi ya ongezeko la wanafunzi. Taasisi pia imeendelea kuboresha mitaala yake ili iendane na mahitaji ya soko na kujenga wahitimu wanaolenga katika kujiajiri,” amesema Dkt. Nyoni.