NA DENIS MLOWE, KYELA
MWANJILISTI, Ambokile Mbwaga ametoa msaada kwa baadhi ya watoto yatima 30 walioko katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, ikiwa ni kurudisha faida baada ya kufanya mauzo ya kitabu chake cha ‘Yesu ni Mwalimu’ wenye thamani ya shilingi milioni 1. 2
Akikabidhi msaada huo ikiwemo fedha taslimu sh. 30,000 kwa kila mtoto kwa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela , Katule Kingamkono, Mwinjilisti Mbwaga alisema kuwa ameamua kutoa misaada hiyo kwa watoto hao wenye mahitaji kutokana na kufata maagizo ya Mungu kutoka katika kifungu cha biblia cha ‘ KUTOKA’ – 22- 24 ambapo umegusia kwa kiasi kikubwa kuhusu wajane na watoto yatima.
Alisema imekuwa kasumba kwa watu wengi kuwasahau watoto yatima na wanaohitaji msaada kwa kuiachia serikali peke yake hivyo baada ya kupata maono ya nini kifanyike alifungua akaunti benki na kuanza kuweka asilimia kumi ya mapato ya kitabu ambacho aliandika ili kila mwaka iweze kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
“Huu ni mwanzo tu wa kuwasaidia watoto hawa na naomba sana jamii iweze kuwasaidia watoto hawa misaada mbalimbali watambue kuwa kuna watu wako nyuma yao na wanawapenda sana na kama unavyoona watoto wamefurahi kuona tunawapatia misaada mbalimbali.” Alisema Mbwaga.
Mwinjilisti Mbwaga alitoa wito kwa watu mbalimbali na mashirika na watu binafsi kujitokeza kutoa misaada kwa watoto hao ili kujengea imani ya kutoona kama wanatengwa katika jamii inayowazunguka na kuwafanya waone maisha yao wako pamoja na jamii inayowazunguka.
Mbwaga alisema kuwa licha ya kukabidhi fedha 30,000 kwa kila motto alitoa sukari kwa kila motto kilo mbili mbili, mchele, sabuni na madftari kumi ambayo wadau mbalimbali walichangia kununulia madaftari hayo.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela, katule Kingamkono alimshukuru mwinjilisti Mbwaga na kusema kuwa licha ya kuonekana msaada mdogo kwa watoto hao lakini misaada kama hiyo ambayo imekuwa ikisadia watoto kujikimu katika mahitaji yao ya kila siku imekuja katika wakati mwafaka sana.
Kingamkono alisema kuwa ni jambo la kushangaza sana kwa mzee ambaye angeweza kutumia fedha yake na familia kuwakumbuka watoto yatima hali ambayo mbele ya mwenyezi Mungu ni thawabu kubwa na kuna umuhimu mkubwa wa watu wengine kuiga tabia aliyoionyesha mwinjilisti Mbwaga.
Alisema kuwa kama halmashauri imepata funzo kubwa na watahakikisha wanafanya jambo kama hilo kwa watoto hao kwani kwa eneo la Kyela kuna watoto yatima 10,000 lakini waliopatiwa msaada ni 30 hivyo kuna umuhimu wa kufanya jambo kubwa zaidi kwa watoto hao ili kuwagusa wengi zaidi.
Kwa upande wao mmoja ya watoto hao aliyezungumza kwa niaba ya watoto wenzake,Angela Lesimani alimshukuru Mwinjilisti Mbwaga na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuwakumbuka katika kuwapatia misaada mbalimbali.