……………………………………………….
Halmashauri ya Nyasa tarehe 2/11/2021 imeanza maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania, kwa kufanya Mdahalo wa kuangalia maendeleleo yaliyofanyika Kabla ya Uhuru na baada ya Uhuru, mdahalo uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Limbo Wilayani Nyasa.
Mdahalo huo umewahusisha wazee maarufu, wanafunzi walimu wa shule za msingi na Sekondari , na wakuu wa idara wa Wilaya ya Nyasa na Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Kanali Laban Thomas.
Akifungua Mdahalo huo Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, amesema Serikali imetoa maelekezo jinsi ya kusherekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wananchi kuchangia miradi ya maendeleo na lengo la kufanya hivi ili wananchi waweze kufahamu kabla ya Uhuru hali ilikuaje na Baada ya Uhuru mambo yaliendeleaje na kwa sasa wapi tunakoelekea.
Ameongeza kuwa, tunakila sababu ya kuwashukuru wazee wetu waliopigania Uhuru kwa kuwa walitukomboa kimawazo na kifikra hali iliyotufanya tupige hatua kimaendeleo hasa kwenye miundombinu ambayo hii leo tunayo kama vile Umeme, maji, Barabara na Reli, pamoja na usafiri wa uhakika wa majini miundombinu inayotumika kutuletea maendeleo.
Ametoa Mfano kabla ya Uhuru hatukuwa na miundombinu inayijitosheleza lakini kwa sasa unaweza kutembea kuanzia Nyasa hadi mwanza na Dar es salaam kwa kutumia barabara ya Lami. Aidha kwa upande wa Elimu amesema elimu ilitolewa kwa upendeleo hasa kwa watoto wa machifu pekee na wanawake walikuwa hawasomi kabisa lakini kwa sasa elimu inatolewa kwa wote bila upendeleo.
Aidha amewataka wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuthamini mchango wa Mnyasa mwenzetu Oscar Kambona ambaye alikuwa mpigania Uhuru wa Tanganyika na kuwataka wananchi wote wakiwa wanasherekea waweze kuwakumbuka mashujaa akiwemo Mw Julius K Nyerere na kujitokeza kwa wingi kushiriki miradi ya Maendeleo.
Aidha katika Mdahalo huo mada mbalimbali Ziliwasilishwa zikiwemo,mbinu zilizotumika kupata uhuru,Maendeleo ya Tanzania baada ya Uhuru, Nafasi za Vijana katika kulinda na Kudumisha Uhuru wa Tanzania , Mchango wa Historia ya jamii husika katika Uhuru wa Nchi na Mafanikio mbalimbali yaliyoletwa na Serikali baada ya Nchi kupata Uhuru hadi sasa.
Aidha wawasilishaji wa Mada hizo wameisifu Serikali ya Tanzania baada ya Uhuru ambao wameweza kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kulinda Uhuru wenye Demokrasia na kulinda amani inayowawezesha wananchi kufanya kazi za maendeleo.
Aidha vijana wametakiwa kufanya kazi kwa juhudi na kulinda amani kwa kushiriki na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa hasa za kujenga miundombinu ya shule, zahanati miradi mbalimbali ambayo inatatua kero za wananchi.