Ufundishaji wa aina hii hufanywa kwa ufanisi zaidi na Walimu wa Elimu Maalum na si vinginevyo.
Na Abby Nkungu, Singida
SUALA la kupata elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum bado ni changamoto kubwa kutokana na uhaba wa walimu wenye taaluma ya lugha ya alama na ukosefu wa miundombinu rafiki ya kujifunzia na kufundishia katika shule za msingi zinazotoa elimu jumuishi mkoani Singida.
Hayo yamebainika katika kipindi hiki cha Siku ya Kimataifa ya Watu wenye ulemavu inayoadhimishwa Desemba 03, kila mwaka ili kukuza uelewa kwa jamii juu ya kundi hilo na kuhamasisha misaada ya kiutu, Haki na Ustawi kwa watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
Hata hivyo, wakati dunia ikiadhimisha siku hii, katika shule ya msingi mchanganyiko Mgori mkoani Singida, wanafunzi wenye mahitaji maalum wanasema wanakabiliwa na changamoto kubwa kupata elimu.
Mmoja wa wanafunzi hao, Amiri Mohamed alisema kuwa shuleni hapo hakuna vifaa muhimu vya kujifunzia kwa wenye ulemavu kama vile Mashine au vitabu vya maandishi ya nukta nundu, hali inayosababisha wasioona kutegemea hisani ya wenzao wanaoona kuwasomea maandishi ya kawaida ubaoni ili waweze kuandika kwenye vibao vyao.
“Mtihani unaletwa kwa maandishi ya kawaida kwa wote, wenye mahitaji maalum na wanaoona. Sasa sisi mpaka mwenzio anayeona akusomee ndipo uweze kuandika. Isitoshe, hapo hakuna mwalimu wa lugha ya alama ambaye anaweza kukusaidia” alisema Amiri.
“Hakuna bweni hapa. Tunakolala ni chumba ambacho awali lilikuwa darasa kabla ya kukarabatiwa kuwa Ofisi ya walimu na sasa ndilo ‘bweni’ letu” alisema Obed Williard, mwanafunzi mwingine.
“Mimi angalau nina uoni hafifu lakini wapo wenzangu ambao hawaoni kabisa. Tunaishi kwenye hili ‘bweni’ ambalo vyoo vyake ni vya nje. Fikiria changamoto zinazowakumba wasioona…..Wanaweza kuumwa na wadudu wenye sumu, nyoka au hata kudhuriwa na watu wabaya”
Mwalimu wa Kitengo cha elimu maalum katika shule hiyo, Hemed Kilango anakiri kukabiliwa na changamoto kubwa katika kuwafundisha watoto hao kwani hakuna vifaa muhimu na bajeti yao ni ndogo kiasi kwamba haiwezi kununua hata kofia, miwani ya jua au mafuta ya ngozi kwa wanafunzi wenye ualbino.
Ofisa elimu Maalum katika Halmashauri hiyo, Huruma Funda alisema kuwa wanahitaji jumla ya walimu 20 wa elimu maalum lakini waliopo ni sita tu, wawili kati yao wakiwa ni wa lugha ya alama.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Elia Digha anasema halmashauri yake ilikwisha kuomba walimu wa elimu maalum kutoka Serikali Kuu lakini walijibiwa kuwa idadi ya walimu wa aina hiyo ni ndogo; hivyo wasubiri hadi hapo watakapopatikana, ndipo watapatiwa.
Hivi sasa Serikali inatekeleza Sera ya elimu Jumuishi inayotaka wanafunzi wenye mahitaji maalum na wenye ulemavu wa aina mbalimbali kusoma na wenzao katika shule moja bila kubaguliwa.