Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Wakazi wa Mji wa Kirongwe wilayani Rorya mkoa wa Mara wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani humo jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa na Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka (katikati) wakitoka ofisi za Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato kwa upande wa Kenya eneo la mpaka wa nchi hizo mbili alipofanya ziara katika kijiji cha Kirongwe wilayani Rorya mkoa wa Mara jana.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Kirongwe wilayani Rorya mkoani Mara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake mkoani Mara
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya idara ya Uhamiaji iliyopo mpaka wa Tanzania na Kenya katika kijiji cha Kirongwe wilaya ya Rorya mkoani Mara
…………………………………………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM RORYA
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoa wa Mara Shilingi Bilioni moja kwa ajili mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika wilaya hiyo na kiaumbele kikubwa ni eneo la mkakati la mji wa Kirongwe uliopo mpaka wa Tanzania na Kenya.
Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kirongwe kilichopo kata ya Bukura wilayani Rorya mkoa wa Mara akiwa katika zira ya siku moja mkoani humo.
Hata hivyo, Dkt Mabula alisisitiza kuwa, wakati wa kuupanga upya mji huo wa Kirongwe kupitia mradi wa KKK hakuna eneo la mwananchi litakalochukuliwa bila ya kulipwa fidia.
‘’Serikali ya Rais Samia imetoa shilingi Bilioni moja kama mkopo kwa ajili ya upangaji maeneo mbalimbali wilayani Rorya ikiwemo kuupanga vizuri mji wa Kirongwe uliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya na lazima fidia ilipwe kabla ya kuchukua maeneo ya wananchi ‘’ alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kupitia mradi huo mji wa Kirongwe utapangwa vizuri na kuainishwa maeneo ya makazi, uwekezaji, viwanda pamoja na huduma za jamii na kusisitiza kuwa upangaji huo ni vyema ukazingatia pia makundi maalum kama vile wamachinga na mamalishe.
Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Fredy Kyalawa alieleza kuwa, fedha walizopatiwa halmashauri ambazo ni za mkopo zitatumika kupanga maeneo katika wilaya ya Rorya na kipaumbele ni eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya katika mji wa Kirongwe.
‘’fedha tuliyopewa tutaitumia kupanga na kupima maeneo mbalimbali katika wilaya yetu ya Rorya na kipaumbele ni eneo la mkakati la mji wa Kirongwe ambapo huko tutalipa fidia na kufanya urasimishaji makazi holela kwa takriban viwanja 5000 na baada ya hapo tutaenda maeneo mengine kama Shirati, Utegi, Mika na Kinesi’’ alisema Kyalawa.
Kwa upande wao, wananchi wa Kirongwe kupitia mkutano na Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula walieleza kuwa pamoja na mpango wa upangaji upya mji huo kuna hatari wakazi hao kuwa watazamaji kwa fursa zitakazokuja kutokana na changamoto kadhaa wanazopata ikiwemo ile wanayopata wakati wa kufanya shughuli zao za uvuvi.
‘’Tunashukuru kwa serikali kuamua kuendeleza mji wetu wa Kirongwe ila kuna hatari ya sisi kuwa watazamaji maana hivi sasa hatuna amani katka eneo la ziwa, wakenya wanasema wamenunua ziwa tunaomba kilio chetu ukipeleke kwa Rais Samia’’ alisema Samson Sabanya mkazi wa kijiji cha Kirongwe.
Naibu Waziri Dkt Mabula aliwaeleza wananchi wa eneo hilo kuwa ataziwasilisha changamoto zao kwa mawaziri wa Uvuvi na Mifugo pamoja na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ili ziweze kushughulikiwa haraka na wao wafaidike na fursa zitakazopatikana wakati wa kuuendeleza mji huo wa Kirongwe.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula alitembelea mpaka wa Tanzania na Kenya ambapo katika kuhakikisha eneo hilo linakuwa na taswira nzuri kwa upande wa Tanzania, alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuharakisha mchakato wake wa kujenga jengo kubwa la ofisi na biashara litakalojumishga taasisi zinazotoa huduma eneo la mpakani kama vile idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Niseme tu ukweli hali ya ofisi zetu hizi hairidhishi ukilinganisha na wenzetu kwa upande wa Kenya eneo la Migori ambapo wana majengo mazuri. Ila nafarijika kusikia NHC inatarajia kujenga jengo kubwa hapa ambalo nina uhakika litakwenda kubadilisha mandhari ya eneo hili niwaombe Shirika la Nyumba kuchangamkia fursa hii itakayotoa fursa kwa wawekezaji wengi kuwekeza hapa” Alisema Dk. Mabula
Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka alisema kuwa, kufuatia Serikali kutoa Bilioni moja kwa ajili ya upangaji na upimaji sasa wilaya nzima ya Rorya inaenda kufunguka kimaendeleo na kuongeza kuwa miji ya Shirati, Utegi na Kinesi nayo inaenda kufunguka kimaendeleo.
‘’Ndugu zangu muda siyo rafiki ili wote kuwa na lugha moja tutakaa kikao cha pamoja na wadau kuona namna tutakavyoweza kwenda fursa hii tuliyoipata , unapowekeza katika ardhi lazima upate mafanikio maana ardhi ndiyo kila kitu’’ alisema Chikota akizungumza katika kikao cha wadau na Naibu Waziri wa Ardhi.