Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Staricko Meshack akizungumza na Wanajumuia wa Chuo Kikuu Iringa wakati msafara wa kuadhimisha siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia ukiwa chuoni hapo.
Wanajumuiya wa Chuo Kikuu Iringa wakichangia mawazo kuhusu ukatili wa kijinsia wakati msafara wa kupinga Ukatili wa Kijinsia ulipopita chuoni hapo katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili huo.
Baadhi ya wananchi na wanachuo wa Chuo Kikui Iringa wakifuatilia mjadala na matukio mbalimbali wakati msafara wa kupinga Ukatili wa Kijinsia ulipopita chuoni hapo katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili huo.
………………………………………………………..
Na Witness Masalu, Iringa.
Wakati Tanzania ikiwa ndani ya kipindi cha maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, imebainika kuwa asilimia 33 ya wanavyuo nchini wamekumbana na ukatili wa kijinsia.
Hayo yamebainika katika msafara wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia unaoendelea ukishirikisha watumishi wa sekta mbalimbali Serikalini na wadau wa Maendeleo .
Akizungumza katika msafara huo kwenye Chuo Kikuu cha Iringa Dkt. Othman Ahmed kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema idadi ya wanavyuo wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ni kubwa hali ambayo haiwezi kuvumiliwa.
Amesema katika kila wanavyuo watatu, mmoja kati yao ni mhanga wa vitendo vya ukatili.
“Kati ya kundi la watu watatu, mmoja wao ni mhanga wa ukatili wa kijinsia, hivyo jamii iendelee kukemea vikali vitendo vyote vya unyanyasaji kijinsia” alisema
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Staricko Meshack amesema Serikali imetoa mwongozo unaoelekeza vitu vya msingi vinavyotakiwa kutekelezwa endapo mtu anafanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo kuanzishwa kwa madawati ya jinsia Vyuoni”
Naye Dennis Lekayo kutoka Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU amewaonya
Wanafunzi wanaotumia wenzao kama chambo dhidi ya walimu wao kwa lengo la kuripoti taarifa za rushwa na hivyo, kufikishwa TAKUKURU.
”Kumekuwa na tabia ya wanavyuo kutafuta wanafunzi ambao wanatumika kama chambo kuwakamata kuwatega walimu wenye misimamo mikali ili wakamatwe na waondolewe Vyuoni,hii si nzuri” alisema
Happy Kimaro kutoka Jeshi la Polisi, Arusha, amesema Madawati ya jinsia yalioanzishwa yanatakiwa kutumika ipasavyo kwani madawati hayo yanafanya kazi kwa kuzingatia usiri.
Novemba 25, mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizindua Kampeni ya maadhimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili na kuelekeza kuazishwa kwa madawati ya Jinsia katika vyuo vya Kati na vyuo Vikuu sambamba na kuanzishwa kwa madawati hayo katika shule za Msingi na Sekondari ikiwa ni njia mujarabu ya kukabiliana na ukatitili nchini.