*****************************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
KATIKA kuelekea miaka 60 ya uhuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kesho ,Desemba 3,kuzindua kiwanda cha kutengeneza nyaya za mkongo wa mawasiliano cha Raddy Fibre Manufacturing (T) Ltd kilichopo wilaya ya Mkuranga.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Abubakari Kunenge alisema , kiwanda hicho ni kikubwa cha nne Barani Afrika cha kutengenezea nyaya zinazotumika kutengeneza mkongo wa mawasiliano.
Alieleza,kiwanda hicho ni moja ya viwanda vikubwa Afrika baada ya vile vya Misri, Algeria na Afrika ya Kusini vinavyotengeneza teknolojia hiyo na kitatoa huduma kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
“Tunamshukuru Rais kwa kutupa heshima ya kuja kwetu kuzindua kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya kuelekea miaka 60 ya Uhuru,” alisema Kunenge.
Alisema kuwa mbali ya kutembelea kiwanda hicho atasimama eneo la Vikindu na kuzungumza na wananchi.
“Atazungumza na wananchi, viongozi wa kisiasa, wazee maarufu, viongozi wa dini na watu mbalimbali,”alisema Kunenge.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kumsikiliza ujumbe atakaowapa juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo.