Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba (suti ya blu) akitazama namna wataalam wa afya wanavyotoa elimu ya hamasa kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani iliyofanyika kimkoa kijiji cha Ilemba Sumbawanga.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Donald Nssoko akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kijiji cha Ilemba Wilaya ya Sumbawanga jana.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Alli Rubeba (kulia) akisoma taarifa ya mkoa kuhusu hali ya maambukizi ya VVU jana wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI iliyofanyika kijiji cha Ilemba Sumbawanga .Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa UKIMWI mkoa Dkt. Kinahi Uwezo .
Mkazi wa kijiji cha Ilemba Wilaya ya Sumbawanga Desdery Malocha akichangia damu jana ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya UKMIWI Duniani.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa).
***************************
Mkoa wa Rukwa kwa ushirikiano na shirika la Walter Reed umefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka asilimia 6.2 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 4.4 mwaka 2016/2017.
Mafanikio hayo yamebainishwa jana (01.12.2021) na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Joseph Mkirikiti kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani iliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Ilemba wilaya ya Sumbawanga.
Waryuba katika hotuba yake alisema kufuatia mafanikio hayo mkoa umeweza kuwatambua na kuwafikishia huduma watu 34,664 wanaoishi na maambukizo ya VVU/UKIMWI ambapo hadi Juni mwaka huu watu 28,410 walikuwa wamepima na kutambulika kuwa na maambukizi.
“Watu 28,283 kati ya 28,410 tayari wameunganishw kwenye huduma za dawa ambayo ni sawa na asilimia 99.6 huku watu 19,830 walikuwa na kiwango kikubwa cha kufubaa kwa virusi vya Ukimwi “ alisema Waryuba.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ally Rubeba alisema kutokana na ushirikiano mzuri na wadau umefanikiwa kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma na malezi kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (CTC) kutoka 31 mwaka 2015 hadi vituo 99 Juni 2021.
Rubeba aliongeza kusema mikakati ya mkoa wa Rukwa katika kipindi cha mwaka 2020/21 ni kuwapima watu wenye sifa za kupimwa VVU 151,205 ambapo utekelezaji wake kufikia Juni 2021 umefikia wateja 120,555 sawa na asilimia 80 huku wateja 3,642 sawa na asilimia 3 wakipatikana na maambukizi.
Katika hatua nyingine Rubeba alisema mkoa umefanikiwa kufanyia vipimo vya ufanisi wa kufanyia kazi figo na maini kwa WAVIU bila malipo hatua inayosaidia kwenye malezi ya wagonjwa.
Katika maadhimisho hayo wananchi wa Kijiji cha Ilemba walipa fursa ya kupata vipimo vya magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari, mapigo ya moyo, saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama na tohara kwa wanaume
Aidha wananchi walijitolea kuchangia damu ambapo kijana Desdery Malocha wa kijiji cha Ilemba alisema amejitolea damu ili iweze kwenda kuokoa maisha wa watanzania hususan akina mama wajawazito wanapata shida wakati wakijifungua.
”Nimejitolea kuchangia damu hii ili ikawasaidie wahitaji kwenye hospitali zetu hususan akina mama wajawazito “alisema Malocha.
Akitoa salamu za wananchi wa Kalambo, Mkuu wa wilaya hiyo Tano Mwera alitoa wito wa watu wote ambapo tayari wanatambua hali zao za maambukizi kuendelea kuwa na ufuasi mzauri wa huduma za matibabu na dawa ili wawe na uhakika wa kuishi muda mrefu.