………………………………………………..
*Asema watoto wa kike wapewe mbinu za kukabiliana na mimba za utotoni na VVU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa walimu kuendelea kuimarisha huduma ya unasihi ili kuwawezesha wanafunzi hasa wa kike kupata stadi za maisha ambazo zitawapa maarifa na mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo mimba za utotoni na maambukizi ya VVU.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali inaunga mkono tamko lililotolewa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeweka wazi azma yake ya kuleta usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa elimu kwa kuruhusu watoto wa kike waliopata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
Mhe. Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumatano, Desemba Mosi, 2021) wakati alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Ruanda-Nzovwe Mkoani Mbeya. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Zingatia Usawa. Tokomeza Ukimwi. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko.”
“…Serikali imeendelea kuimarisha mipango mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kujifunza kwa wanafunzi hususan wa kike ikiwemo kuongeza shule mpya za sekondari za wasichana za bweni kote nchini ili kutoa fursa kwa mtoto wa kike kukamilisha mzunguko wake wa masomo na hivyo kuweza kutimiza ndoto zake.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imeshaweka mipango madhubuti na mazingira mazuri ya mapokezi ya wasichana ambao walikatiza masomo kutokana na ujauzito. “Vilevile, Serikali imeendelea kuhakikisha shule za msingi zinajengwa kila kijiji na shule za sekondari kila kata ili kupunguza umbali na kuondoa vishawishi hasa kwa wanafunzi wa kike.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, shilingi bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya kujenga shule 10 kati ya shule 26 zilizo katika mpango. Shule hizo zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 1,000 hadi 1,200.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa zimesalia siku nane tu ili nchi ifikie kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru na kwamba namna bora ya kuadhimisha siku hiyo ni kwa Watanzania kujitathmini kila mmoja amelifanyia nini Taifa na kwa kiasi gani atashiriki katika kuliletea maendeleo.
Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania wote wajitokeze kwa wingi katika siku ya kilele ili waweze kusherehekea kumbukizi ya Uhuru wa nchi yao kwa pamoja. Maadhimisho ya siku ya Uhuru Kitaifa yatafanyika katika uwanja wa Uhuru Mkoani Dar es Salaam siku ya tarehe 9 Desemba, hivyo amewakaribisha Watanzania wote kushiriki katika tukio hilo.