……………………………………………………
*Asema kauli, vitendo na mitazamo ya ubaguzi kwa kundi hilo havikubaliki
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kuwanyanyapaa na kuwabagua Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) kwa kuwa vitendo, kauli au mitazamo ya unyanyapaa na ubaguzi kwa kundi hilo havikubaliki.
“Kumekuwa na madai kuwa watumishi wa afya wana tabia za unyanyapaa na kuvujisha siri za WAVIU wanapotoa huduma katika vituo vyetu vya tiba na matunzo kwa WAVIU. Vitendo na tabia hizi ziripotiwe mara moja pindi vitakapotokea.”
Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Desemba Mosi, 2021) wakati alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Ruanda-Nzovwe mkoani Mbeya. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Zingatia Usawa. Tokomeza Ukimwi. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema nchi ina sheria ya UKIMWI ambayo imefanyiwa marekebisho kadhaa ili kuhakikisha kuwa huduma za VVU na UKIMWI zinamfikia kila mlengwa. “Ninaelewa kuwa unyanyapaa na ubaguzi kwa WAVIU bado ni changamoto kubwa katika jamii zetu.”
“Hii inatukwaza na kurudisha nyuma juhudi za mwitikio wa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini. Mfano baadhi ya watu wanaoishi na VVU wanaona aibu kutumia huduma za VVU na UKIMWI zilizopo kwa sababu ya unyanyapaa na ubaguzi, hasa katika maeneo ya vijijini.”
Akizungumzia kuhusu kaulimbiu ya maadhimisho hayo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kaulimbiu hiyo ni thabiti kwa sababu inatoa muelekeo bora wa jinsi ya kuondoa changamoto zilizopo ili kupata matokeo bora zaidi, ikimaanisha kwamba kila wanachokifanya kwenye miradi na afua za udhibiti UKIMWI nchini usawa lazima uzingatiwe.
“Usawa unahitajika kwenye mahitaji ya msingi ya makundi mbalimbali kwani UKIMWI hauchagui umri, jinsi wala rika. Hivyo kaulimbiu hii inatukumbusha wajibu wetu wa kuzingatia utoaji wa huduma kwa makundi yote ambayo ni pamoja na watoto, vijana, wanawake, wasichana, wanaume, wazee, watu wenye ulemavu na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi zaidi.”
Hivyo, Waziri Mkuu amesema ili kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu hiyo uwekezaji unatakiwa uzingatie mahitaji halisi kwa kila kundi, mazingira halisi na uhatarishi uliopo. “Licha ya hayo haki za binadamu pia zizingatiwe ili huduma zote zinazohusu masuala ya VVU na UKIMWI zitolewe kwa usawa unaohitajika.”
Kadhakika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau wote kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na Wadau wa Maendeleo kuhakikisha uendelevu wa afua za VVU na UKIMWI nchini kwa kuweka mikakati ya kukusanya rasilimali za ndani.
“Serikali yetu sikivu itaendelea kutenga bajeti na kutafuta vyanzo endelevu vya kutunisha mfuko Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI kadiri uchumi utakavyoruhusu. Natoa agizo kwa TACAIDS kwa kushirikiana na Wizara ya fedha na Mipango na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuangalia utaratibu mzuri na wa uhakika wa kutunisha mfuko huu.”
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema huduma za ARV kwa watu wanaoishi na VVU zinaendelea kuimarishwa kwa kuhakikisha kuwa wanaogundulika wanaishi na VVU wanapaswa kuanza kutumia ARV mapema pamoja na kuzingatia ufuasi sahihi wa huduma hizo.
Amesema katika kudhibiti kuenea kwa maambukizo mapya ya VVU, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kutekeleza mkakati wa nne wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI kwa kushirikisha sekta zote nchini. Mkakati huo wa mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023 umelenga kupunguza maambukizi mapya ya VVU na vifo vinavyohusiana na UKIMWI.
“Kwa upande mwingine mkakati wa nne wa Taifa unaelekeza utekelezaji wa program za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na upimaji wa hiari. Huduma hizi hutolewa chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto huku wadau wengine wakifanya uhamasishaji kwa wananchi kuziendea huduma zinazotolewa.”
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA), Bibi Leticia Maurice ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa maono na jitihada zake za kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya afya.
Mwenyekiti huyo wa NACOPHA ameongeza kwa kusema kuwa Watu Waishio na Virusi vya UKIMWI wanamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuhakikisha wanapata dawa zao za ARV bila malipo, hivyo kuwawezesha kuishi na kuendesha shughuli zao za kinaendeleao ipasavyo.