Mkuu wa mkoa wa Arusha akizungumza katika maadhimisho hayo jijini Arusha
Baadhi ya wananchi wakiwa katika siku ya maadhimisho ya ukimwi duniani yaliyofanyika katika uwanja wa soko la Kilombero mjini hapa.
…………………………………………..
Happy Lazaro, Arusha.
Maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika wilaya ya Arusha yameongezeka kutoka asilimia 2.3 kwa mwaka 2019/2020 hadi asilimia 2.8 katika kipindi cha mwaka 2020/2021.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ya wilaya ya Arusha,Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya jiji la Arusha,Tajiel Mahega ameeleza kuwa kiwango hicho kimeongezeka kutokana na zoezi la upimaji wa makundi maalumu ikiwemo baadhi ya vijana wanaoathirika na madawa ya kulevya.
“Makundi mengine ni pamoja na madada poa ikiwa sababu nyingine ni kuongezeka kwa vigezo vya upimaji kwa ufanisi hali iliyosababisha watu wengi kujitokeza kupima na kubainika kwa ongezeko hili,”amesema Mahega.
Mahega amesema kuwa, pia kuna changamoto ya jamii kutohudhuria kliniki ya tiba na mafunzo ambayo hupelekea kushindwa kuchukua dawa na wagonjwa wengine kujnyanyapaa wenyewe kwa kuhofia kujulikana na watu.
Hivyo amesema katika suala hilo wanaihasa jamii kuwa kupata ugonjwa wa ukimwi sio mwisho wa maisha ila kwa mtu yeyote aliyepata maambukizi anapaswa kujikinga na kuwakinga wengine pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya.
Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongella amesema ni vyema makundi yote wakafuata masharti na maelekezo ya wataalamu katika kujikinga na ugonjwa huo ili kuongeza uzalishaji na maendeleo ya nchi katika hali ya usalama wa kiafya.
“Kwanza tujitahidi kujikinga ,kujizuia ,kujihusisha na ngono zembe kwani bado maambukizi mengi yapo hivyo mshikamano wa madhehebu pamoja na serikali utatufanya tuondokane na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kwa kuweza kuyakabili,”amesema Mongella.
Nao baadhi wa wakazi wa jiji la Arusha wamesema changamoto ni elimu hali ambayo huwafanya watu kutojiamini ikiwa wengine uoga wa matumizi ya nyenzo za kujikinga kutokana na imani haba.