……………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Kitabu kinacholenga kusaidia Wathibiti Ubora wa Shule katika shughuli zao za Ukaguzi wa Shule kimezinduliwa rasmi Leo ADEM Bagamoyo, kikiwa na mantiki ya kukuza uelewa juu ya Uhakika wa Ubora katika Sekta ya elimu.
Mgeni wa heshima katika uzinduzi huo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taaluma, Utafiti na Ushauri Weledi kutoka Chuo cha Wakala wa Maendeleo ya Elimu (ADEM) Dkt. Alphonce J. Amuli, amesema kitabu hiko kimeandaliwa na kutolewa wakati sahihi ambao Mashirika mengi Duniani kote ikiwa ni pamoja na Taasisi za elimu zinajitahidi kuhakikisha zinatoa huduma bora za elimu.
“Ni wakati sahihi kwa Wasimamizi wa Elimu, na Maafisa wanaofanya Uthibiti wa elimu kutumia kitabu hiki kama chombo cha mabadiliko katika kuhakikisha ubora katika sekta ya elimu nchini “ Amesema Dkt. Amuli.
Nae Mwandishi wa kitabu hiko Dkt. Mwita Abel Mkami, ambaye pia ni Mkufunzi katika Chuo cha ADEM Bagamoyo, akizungumza katika uzinduzi huo amesema utoaji wa huduma bora za kielimu, huanza na ukaguzi wa ubora wa elimu inayotolewa.
Njia hii husaidia sana juu kubainisha kasoro zilizopo katika utoaji wa elimu bora ikiwa ni pamoja na kutofuata viwango vilivyowekwa wakati wa utoaji wa elimu bora, hivyo miongozo iliyomo katika kitabu hicko itawasidia Wathibiti Ubora wa Elimu wakati wa kutekeleza Shughuli zao za Ukaguzi na Uthibiti Ubora wa Elimu ili kupata Shule bora, Elimu bora na Wahitimu bora na kwamba kitabu hiko kina jumla ya Sura tano.