………………………………………………………
NA VICTOR MAKINDA: MVOMERO
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, Halima Okash, ameziomba Asasi za Kiraia (AZAKI) zinazofanya shughuli zake wilayani hapa, kusaidiana na viongozi wa ngazi viongozi wa ngazi mbali mbali pamoja na kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Okash alitoa ombi hilo jana Novemba 30 wakati wa mkutano baina yake na Asasi za Kiraia uliolenga kujadili na kupendekeza mbinu za usuhulishi wa kudumu wa migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani hapa.
“ Pamoja na jitihada kubwa ambazo serikali inafanya kuimaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani Mvomero, lakini bado kuna viashiria vya uwepo wa migogoro baina ya makundi hayo. Nimewaita ndugu zangu wa Asasi za Kiraia mnaofanya kazi zenu wilayani hapa, ili kwa pamoja tujadili na kupendekeza mbinu muafaka ambazo zitasaidia kumaliza kabisa migogoro hiyo. Alisema Okash.
Katika hatua nyingine Okash alizitaka Asasi za Kiraia zinazofanya kazi wilayani hapa kujielekeza katika kutekeleza miradi ambayo ina matokea chanya ya moja kwa moja kwa jamii ili kusukumu kwa haraka gurudumu la Maendeleo ya wilaya ya Mvomero na Tanzania kwa ujumla.