Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 30,2021 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya sekta ya Maliasili na Utalii katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (hayupo pichani) wakati akiwasilisha mafanikio ya Sekta ya Maliasili na Utalii katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 30,2021 jijini Dodoma wakati akizungumzia mafanikio ya Sekta ya Maliasili na Utalii katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
……………………………………………….
Alex Sonna,Dodoma
WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara imefanikiwa kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za maliasili kwa kudhibiti ujangili, uvunaji haramu wa mazao ya misitu na uvamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa, Serikali imeendelea kuweka juhudi katika kulinda rasilimali hizi ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kikosikazi cha Taifa Dhidi ya Ujangili kinachojumuisha wadau wengine.
Pia kuanzisha Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu na kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2014.
Hayo yameelezwa leo Novemba 30,2021 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja,wakati akizungumzia mafanikio ya wizara ya Maliasili na Utalii katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Aidha, operesheni za kiintelijensia zimeendelea kufanyika katika maeneo yaliyohifadhiwa ili kupunguza vitendo vya ujangili na uvunaji haramu wa rasilimali za wanyamapori na misitu.
”Mfano, kwa miaka ya hivi karibuni matukio ya vifo vya tembo kutokana na ujangili yameendelea kuwa chini kutoka tembo 18 mwaka 2016/17 hadi tembo watatu (3) mwaka 2020/21.
Amesema katika miaka ya karibuni hakukuwa na matukio makubwa ya ujangili wa faru kutokana na jitihada mbalimbali zikiwemo kuimarishwa kwa shughuli za doria, utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa jamii na kuimarishwa kwa shughuli za intelijensia katika maeneo ya hifadhi na vijiji vinavyozunguka hifadhi za Taifa.
“Kupitia juhudi hizi, taarifa za ufuatiliaji wa matukio hayo zilizopo zinaonesha kuwa ujangili umepungua kwa takriban asilimia 90. Katika hatua nyingine, Serikali imeendeleza juhudi za kudhibiti maeneo yaliyohifadhiwa kwa shughuli za binadamu kama vile kilimo na mifugo,”amesema.
KUIMARISHA UTANGAZAJI WA VIVUTIO VYA UTALII NCHINI
Mhe.Masanja maesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii nchini, idadi ya Watalii wanaoingia nchini kutoka katika nchi mbalimbali Duniani imeongezeka kutoka 9,847 Mwaka 1960 hadi kufikia watalii 1,527,230 Mwaka 2019.
Mhe.Masanja amesema kuwa kumekuwepo na ongezeko la mapato yatokanayo na watalii, kwa mfano mwaka 1995 mapato yalikuwa Dola za Marekani milioni 259.44 ambapo yaliendelea kuongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2019 kabla ya Ugonjwa wa UVIKO-19.
“Kutokana na jitihada za Serikali katika kukabliliana na ugonjwa wa UVIKO-19 idadi ya watalii imeanza kuongezeka kutoka watalii 620.867 mwaka 2020 hadi kufikia 716,169 mwezi Oktoba 2021,”amesema.
YAPUNGUZA VIWANGO VYA ADA
Aidha, katika kuendelea kujenga mazingira bora ya kuwawezesha wananchi hususan vijana kuanzisha biashara za utalii nchini, Serikali imepunguza viwango vya ada ya leseni kutoka Shilingi za Tanzania sawa na Dola za Marekani 2000 hadi Shilingi za Tanzania sawa na Dola za Marekani 500 kwa magari kuanzia moja hadi matatu.
“Hatua hii imelenga kuongeza ushiriki wa wakala wa biashara za utalii ambao ni wazawa katika biashara za utalii. Kufuatia hatua hiyo, wakala wa biashara za utalii wazawa waliongezeka kutoka wakala 643 hadi kufikia 1,687 sawa na ongezeko la asilimia 162.4,”amesema.
Vilevile,Serikali imefanikiwa kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii katika kutangaza na kuhamasisha utalii wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo, watu wenye mahitaji maalum, vikundi vya kidini, Madereva wa bodaboda na bajaji, mashirika binafsi na ya kiserikali.
Aidha, wananchi wengi wemeendelea kushiriki kwenye shughuli za utalii ambapo ajira takriban milioni 1.6 za moja kwa moja na zile ambazo sio za moja zimepatikana.
UWINDAJI NA VITALU
Aidha,Naibu Waziri Masanja amesema katika kuimarisha shughuli za utalii wa uwindaji Serikali imeanzisha utaratibu wa kuuza vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada kupitia mfumo wa kielektroniki.
Amesema katika awamu nne (4) za mnada wa kugawa vitalu kwa njia ya kielektroniki uliofanyika kati ya Juni 2019 na Mei 2021, asilimia 26 ya vitalu 46 vilivyoingizwa kwenye mnada viliuzwa.
Amesema Mapato yaliyopatikana ni asilimia 84 ya mapato yote ambayo yangepatikana kwa kugawa vitalu vyote 46 bila mnada.
KUONGEZEKA KWA MAZAO MAPYA YA UTALII
Aidha,Naibu Waziri huyo amesema katika kuvutia watalii wengi zaidi na kuongeza siku za mtalii kukaa nchini, Serikali imeendelea kuibua na kukuza mazao mapya ya utalii ambayo yameendelea kufanya vizuri.
Ameyataja mazao hayo kuwa ni ya utalii wa michezo; utalii wa meli (Cruiseship Tourism); utalii wa fukwe; utalii wa mikutano na matukio; utalii wa nyuki (Api-Tourism); utalii wa kihistoria; utalii wa matibabu kwa kuanzia katika Hospitali za Umma za Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa (MOI)
“Pamoja na utalii katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI); utalii wa kilimo (Agrotourism) na Utalii wa Utamaduni. Mathalan, hadi sasa kuna miradi ya ujasiriamali wa utalii wa utamaduni zaidi ya 100 kwa nchi nzima,”amesema.