WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 30,2021 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Baadhi ya Waandishi wa Habari na watumishi wa TAMISEMI wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) wakati akiwasilisha mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.Ummy Mwalimu,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari leo November 30,2021 jijini Dodoma wakati akizungumzia mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu amesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara inavunia kuboresha sekta ya afya,elimu,kuwezesha wananchi kiuchumi pamoja na Ujenzi wa Miundombinu ya utoaji huduma kwa jamii.
Hayo yamesemwa leo Novemba 30,2021 jijini Dodoma wakati akizungumzia mafanikio ya wizara ya TAMISEMI katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Waziri Ummy amesema mweleko wa Wizara hiyo katika sekta ya afya ni Ujenzi na ukamilishaji wa zahanati kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma za afya huku katika elimu kikiwa ni kujenga shule mpya 1,000 za sekondari katika kata zisizokuwa na shule na ambazo zina msongamano mkubwa wa wanafunzi.
MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA ELIMU
Amesema Katika kipindi hiki Elimu ilitolewa kwa watu wachache kwa lengo la kupata maafisa wachache ambao wanaweza kusaidia katika shughuli mbalimbali za utawala na kuandaa watu kwa ajili ya kushika uongozi wa nchi.
Amesema hadi mwaka 1961, kulikuwa na shule za Msingi 3,270 zilizokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 450,626 ambapo amedai Shule hizo ziligawanywa kwa matabaka ya rangi ambapo kati ya Waafrika 9,869,000 wanafunzi 431,056 walipata nafasi ya kusoma katika shule 3,115 na kati ya wananchi Wasio Wafrika 150,000 wanafunzi 19,570 walipata nafasi ya kusoma katika shule 155.
Waziri Ummy amesema kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuiwa na Serikali kuanzia Uhuru hadi sasa mafanikio makubwa yaliyopatikana ni pamoja na idadi ya shule za Msingi za Serikali zimeongezeka kutoka 3,270 mwaka 1961 hadi 16,656 mwaka 2021.
Aidha, idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 486,470 mwaka 1961 hadi 10,687,593 mwaka 2021. Walimu wameongezeka kutoka 9,885 mwaka 1961 hadi 171,993 mwaka 2021.
Amesema Shule za Sekondari zimeongezeka kutoka 39 mwaka 1961 hadi 4,002 za Serikali mwaka 2021.
Vilevile, idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 2,379,945 mwaka 2021. Walimu wameongezeka kutoka 764 mwaka 1961 hadi 87,992 mwaka 2021.
“Shule za Elimu Maalum zimeongezeka kutoka nne (4) za wamisionari (Tabora, Buigiri, Irente na Uhuru Mchanganyiko mwaka 1961 hadi kufikia 746 mwaka 2021.
Aidha, kuna Elimu Jumuishi katika shule zote za msingi. Idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum imeongezeka kutoka 1,000 mwaka 1960 hadi 70,265 mwaka 2021,”amesema.
Amesema Utoaji wa Elimumsingi bila Malipo unazingatia Ibara ya 3.1.5. ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na Ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Waziri Ummy amesema Kiasi cha shilingi bilioni 23.8 zinatolewa kila mwezi kuanzia mwezi Disemba, 2015 kwa ajili ya kugharamia utoaji wa Mpango wa Elimumsingi bila Ada na shilingi bilioni 3.0 zinapokelewa Baraza la Taifa la Mitihani kwa ajili ya shughuli za Mitihani.
Pia, kuanzia mwezi Oktoba 2021 Serikali imepeleka Shilingi bilioni 26.00 kwa ajili ya uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari nchini.
“Kuanzia Disemba, 2015 mpaka sasa Serikali imepeleka jumla ya Shilingi trilioni 1.43. kwa ajili ya kugharamia Mpango wa Elimumsingi bila Malipo. Fedha hizi zimekuwa zikipelekwa katika shule moja kwa moja na kuwafikia wanufaika,”amesema.
Amesema Mpango wa Elimumsingi bila malipo umesaidia kuongeza uandikishaji wa wanafunzi kutokana na kuondolewa kwa vikwazo.
Amesema Katika mwaka 2016 jumla ya wananfunzi 3,335,637 waliandikishwa, kati ya hao wanafunzi 1,013,310 wa elimu ya awali, 1,896,584 wa darasa la kwanza na wanafunzi 425,743 wa kidato cha kwanza.
“Mwaka 2021 jumla ya wananfunzi 3,469,275 waliandikishwa, kati ya hao wanafunzi 1,198,564 wa elimu ya awali, 1,549,279 wa darasa la kwanza na wanafunzi 721,432 wa kidato cha kwanza,”amesema
MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA AFYA
Waziri Ummy amesema Mwaka 1961, kulikuwa na Vituo vya kutolea huduma za Afya 1,343 vilivyokuwa na idadi ya vitanda 18,832 nchini. Serikali za Mitaa ilikuwa inamiliki Vituo vya Afya na Zahanati 737 pekee zenye vitanda 1,795.
“Watumishi wa kada mbalimbali za Afya walikuwa 3,172 kati yao Madaktari walikuwa 580, Madaktari wa Meno 30, Wasaidizi Madaktari wa Meno 19, Wafamasia 50,Wasaidizi Wafamasia 38, Tabibu 402, Wauguzi 1,999, Wateknolojia Maabara 3, Wasaidizi Maabara 49 na Wataalam wa Mionzi 2,”amesema.
Aidha mwaka 1961 watumishi waliofuzu Shahada ya Udaktari walikuwa 400 kati yao Watanzania wakiwa 20 pekeee
Amesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara Zahanati na vituo vya afya vimeongezeka kutoka 737 mwaka 1961 hadi 5,696 (Vituo vya afya 630 na zahanati 5,066) vya Serikali za Mitaa.
“Hospitali zinazotoa huduma zimefikia 142 mwaka 2021 wakati Serikali za Mitaa hazikuwa na hospitali mwaka 1961,”amesema.
Amesema Vituo vya Afya vinavyotoa huduma za upasuaji zimeongezeka kufikia 415 wakati hapakua na kituo kinachotoa huduma za upasuaji mwaka 1961.
MIUNDOMBINU
Waziri Ummy amesema wakati wa Uhuru mtandao wa barabara ulikuwa na jumla ya kilometa 33,600 zilizojumuisha kilometa 16,000 zilizokuwa zikitambuliwa kama Barabara Kuu za Nchi na za Kawaida (Territorial Main and Local Main Roads) na kilometa 17,600 zikiwa ni Barabara za Wilaya (District Roads).
“Hata hivyo mwaka 2006, kulifanyika zoezi la kuhakiki wa hali ya barabara nchini zilizochini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Local Government Roads Inventory and Condition Survey – LG-RICS),”amesema.
MWELEKEO KATIKA BARABARA
Waziri Ummy amesema mwelekeo wa Wizara hiyo katika eneno la barabara ni kuongeza mtandao wa barabara za udongo kuwa za changarawe.
Amesema kwa kipindi cha 2021/22 hadi 2025/26 imepanga kuongeza barabara za changarawe kutoka kilometa 29,116.57 hadi kufikia kilometa 102,358.1.
“Mapango huu unakadiriwa kutumia shilingi trillion 2.974 kwa kipindi cha miaka 5, na katika hatua hii tunamshukur Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya Tarura kutoka shilingi bilioni 271 mwaka wa fehda 2020/21 hadi kufikia bilioni 966.9 mwaka wa fedha 2021/22,”amesema.