********************************
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Mkoa wa Katavi umeelezwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaonyonyesha watoto kutokana na kuwa na asilimia kubwa ya wanawake wanaotegemea shughuli za kilimo katika kuendesha maisha yao
Hayo yameelezwa na Mratibu wa afya ya mama na mtoto mkoa wa Katavi Sista Elida Machungwa.
Sista Machungwa amesema kufuatia shughuli kubwa ya wanawake hao kutegemea kilimo wamekuwa na muda wa kutosha kunyonyesha watoto na kuongeza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wanawake wenye watoto wananyonyesha maziwa yao.
“Hata wakiwa katika kazi za shamba kinamama wanakwenda na watoto wao na hivyo ni rahisi kunyonyesha kila mtoto anapohitaji kunyonya” alisema sista Machungwa.
Ameongeza kuwa unyonyeshaji una faida kubwa kwa mama na mtoto ikiwemo uimarishaji wa afya ya akili katika maendeleo ya mtoto, kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa, kupunguza hatari za utipwatipwa, kupunguza gharama za huduma kwa mtoto na pia kuwalinda kina mama wanaonyonyesha dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti.
Amesema faida za kiafya, kijamii na kiuchumi za unyonyeshaji zinajulikana na kukubalika kote duniani, lakini bado baadhi ya kinamama wanashindwa kunyonyesha kutokana na sababu mbalimbali.
“Mtoto anapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita tangu kuzaliwa kwake lakini kinamama wengine wanashindwa kufanya hivyo kutokana na kuwa wafanyakazi hivyo wanalazimika kurudi kazini mapema kutoka likizo ya uzazi” alisema Machungwa.
Kwa mujibu wa takwimu za UNICEF zinasema ni watoto 4 tu kati ya 10 walionyonyeshwa maziwa ya mama katika miezi sita ya mwanzo ya maisha yao sawa na asilimia 41 ya watoto wote.
Kinamama waliojifungua katika Hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Katavi wamemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa wana mpango wa kunyonyesha watoto kwa kufuata ushauri wa wataalamu
“Kama mimi sina uwezo wa kumnunulia mtoto maziwa kwahiyo nitamnyonyesha maziwa yangu kwanza hayana gharama mama ukishiba vizuri maziwa ni mengi!” alisema Mwasiku Kajala mkazi wa Mwankulu
Shenaiza Abdallah ni muuguzi kutoka Kituo cha Afya Mwangaza amesema wanawake wajawazito wanapohudhuria kliniki wanapatiwa mafunzo mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kunyonyesha maziwa ya mama
Ameeleza kuwa unyonyshaji pia unasaidia kumkinga mtoto na tatizo la udumavu