Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila YusuphMakaburi ya Mwangaza yanayounganisha kata mbili Makanyagio na Majengo. Watu wengi hutumia njia mkato zilizo katika makaburi haya kupita kwenda upande wa pili.
***************************
Na Zillipa Joseph, Katavi
Imeelezwa kuwa uhamasishaji wa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali yenye vichaka vikiwemo viwanja vilivyotelekezwa, na maeneo ya makaburi na viwanja vya michezo katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi umesaidia kupunguza vitendo vya ubakaji vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya watu wakitumia vichaka hivyo kujificha wakati wakifanya uhalifu huo.
Ubakaji huo uliwaathiri zaidi watoto wadogo waliokuwa wakipita katika maeneo hayo wakienda sehemu mbalimbali kama shule ama kutumwa dukani na wazazi wao.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Dawati la Jinsia mkoa wa Katavi SSP Esther Rwechungura ameishauri jamii kupinga ukatili wa kijinsia.
“Jamii lazima jamii ioneshe kuwa inakerwa na haifurahishwi na vitendo hivi. Madawati ya jinsia yaliyopo kwenye jeshi la polisi yanatumika katika kutatua migogoro ya unyanyasaji wa kijinsia, likiwamo suala zima la ubakaji” alisema Afisa huyo wa Jeshi la Polisi.
Ameongeza kuwa kwa mwaka uliopita walikuwa wakipokea matukio matatu hadi sita ya ubakaji na ulawiti kwa watoto walio chini ya umri wa miaka saba kwa wiki tofauti na mwaka huu ambapo ni kati ya mtoto mmoja hadi watatu wanaofikishwa kwenye dawati kwa wili kwa ajili ya matukio hayo.
“Na ukiuliza unasikia alibakwa katika kiwanja cha mpira au makaburini” aliongeza.
Hata hivyo ameitaka jamii kuwaelimisha watoto juu ya mazoea ya kuwaita watoto mchumba kwani wabakaji walio wengi ni watu walio karibu na watoto.
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph amesema kufuatia matukio hayo kuripotiwa mara kwa mara waliamua kusimamia usafi wa maeneo mbalimbali ili kuwanusuru watoto.
“Ulikuwa ukipita kule makaburi ya Mwangaza hata uwe mtu mzima utasisimka majani yalikuwa marefu yanapita kimo cha mtu mzima. Pia tuliongea na watendaji wa mitaa kuhakikisha mapagale yote yanafanyiwa usafi” alisema Jamila
Mkuu huyo wa wilaya yam panda amesema wakati Tanzania ikifikisha miaka 24 ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yenye kauli mbiu isemayo “Ewe mwananchi komesha ukatili wa kijinsia sasa” amewataka wananchi wote kuchukua hatua madhubuti kwa watu wanaofanya vitendo vya ukaili wa kijinsia ili kukomesha vitendo hivyo na kutengeneza usawa na uthamini wa kijinsia.
Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Mpanda wameisifu serikali kwa kusimamia suala la usafi wa mazingira na kusema si tu watoto walikuwa wakipata madhara hata watu wazima walikuwa wakikabwa hasa majira ya usiku.
“Sasa hivi unapita makaburini bila woga maana unaona hadi magari yanayopita upande wa pili, zamani huthubutu kupita ikifika saa mbili usiku” alisema Mwajuma Ali mkazi wa Makanyagio