Wataalam wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wapo mkoani Iringa katika zoezi la kusajili Skimu za Umwagiliaji pamoja na kutoa elimu ya Ada na Tozo kwa viongozi wa vyama vya wamwagiliaji.
Akizungumza na Viongozi wa Skimu ya Mangalali iliyopo Wilaya ya Iringa Vijijini, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mazingira Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw, Fumba Malima amewaeleza viongozi hao kuwa, suala la kulipa Ada na Tozo za Umwagiliaji lipo kisheria na sio hiari na kuwataka viongozi wa Skimu ya Mangalali kusimamia kwa weledi zoezi la ukusanyaji Ada na Tozo za Umwagiliaji ili kuharakisha maendeleo ya sekta ya Umwagiliaji nchini.
“Fedha hizo ndizo zitakazotumika kukarabati Miuondombinu ya Umwagiliaji iliyoharibika katika Skimu zenu, pamoja na kujenga Skimu mpya kufikia Hekta Milioni Moja na Laki mbili mwaka 2025, kama ilani ya chama Tawala inavyoelekeza”.
Kwaupande wake Afisa Kilimo kutoka Tume Bi,Restuta Mushi, ametumia fursa hiyo kuwaelimisha viongozi hao, njia inayotumika kulipia Ada na Tozo za Umwagiliaji ambapo mhusika anapaswa kufanya malipo kupitia namba maalum ya Malipo itakayotolewa na idara ya uhasibu ya Tume, lakini pia amewapa fomu maalum itakayorahisisha zoezi la kuhamisha fedha za Ada na Tozo kwenda akaunti ya Mfuko wa Umwagiliaji mara baada ya chama hicho kuingia makubaliano na benki wanayohifadhia fedha zao.
Mtaalam wa masuala ya Umwagiliaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bw,Bonaventure Mkude amesema makusanyo ya Tozo katika Skimu hiyo ni yakusuasua kwasababu hapo nyuma hakukuwa na matumizi ya sheria ya Umwagiliaji, hivyo kulipa faini ya Tsh, milioni moja au kwenda jela mwaka mmoja, ama vyote kwa pamoja, itasaidia zoezi la ukusanyaji wa Ada na Tozo za Umwagiliaji kufanyika kwa wakati na zoezi hilo kuwa endelevu kwakuwa ni takwa la kisheria.
Mwandisi wa Umwagiliaji wa Tume Mkoa wa Iringa, Bw, Onesmo Kahoggo amewashauri viongozi hao wa Skimu ya Mangalali kumshirikisha katika vikao vyao na wakulima ili aweze kufafanua kwa karibu zaidi umuhimu wa kulipa Ada na Tozo za Umwagiliaji sanjari na faida watakazopata wakulima wa Skimu hiyo kutokana na michango yao kila msimu wa mavuno.
Viongozi wa Skimu hiyo wameahidi kujisajili Tume ya Taifa ya Umwagiliaji pamoja na kulipa Ada na Tozo kwa wakati kwa mujibu wa sheria.
Skimu ya Mangalali ina jumla ya wanufaika 250.
Kaimu Mkuu wa kitengo cha Mazingira Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (Wa pili kushoto ) Bw, Fumba Malima akitoa elimu kwa Viongozi wa chama cha Wamwagiliaji Skimu ya Mangalali kuhusu sheria ya Umwagiliaji na takwa la kisheria la kulipa Ada na Tozo. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Skimu ya Mangalali Bw, Piero Ngahega, akisikiliza kwa makani.
Kushoto kwa Bw, Fumba Malima ni Bi, Restuta Mushi afisa kilimo Tume na anayefuatia ni Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Iringa Bw, Onesmo Kahoggo.
Bw, Bonaventure Mkude, Mtaalam wa Masuala ya Umwagiliaji Halmashauri ya Wilaya ya Iringa akichangia mawazo yake kuboresha mikakati ya ukusanyaji wa Ada na Tozo za Umwagiliaji.
Picha za kilimo cha Mahindi, Nyanya na Mbogamboga katika Skimu ya Mangalali Iringa Vijijini.