Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga alipofika kusikiliza na kutatua changamoto zao. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo, Calist Lazaro.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.
Watumishi na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mji na DC wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi alipofika kuzungumza nao ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kuzungumza na watumishi wa umma pamoja na kutatua changamoto zao.
Mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga akimueleza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi changamoto yake inayomkabili.
…………………………………………………..
BADILIKENI! Ni kauli ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi kwa Maafisa Utumishi nchini wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Korogwe na Handeni ambapo amewataka Maafisa Utumishi hao kuacha tabia ya kujifanya miungu watu na badala yake wafanye kazi ya kuwahudumia watumishi wa umma kama ambavyo kanuni na sheria zinawaelekeza.
Ndejembi ametoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mji na DC wakidai malimbikizo ya mishahara yao.
“Ndugu zangu watumishi Ofisi ya Rais Utumishi imekua ikishughulikia madai yote ya watumishi kwa wakati niwaeleze ukweli mpaka kufikia Ijumaa tayari tulikua tumeshapitia fomu zote, changamoto iliyopo ni ya Maafisa Utumishi wetu huku chini kutofuatilia madai ya watumishi wao wizarani.
Wote mmeshuhudia Maafisa Utumishi hawa wanasema mara ya mwisho kufuatilia ilikua Machi mwingine Agosti sasa kwa staili hii watumishi mnaweza kudhani shida iko kwetu wizarani kumbe ni kwa hawa Maafisa Utumishi, hivyo ninawapa siku mbili wafike wizarani Dodoma kuja kufuatilia fomu za watumishi wanaodai na kama kuna maelekezo ya kurekebisha wawaite watumishi wajaze ili ziturudie kwetu muweze kulipwa,” Amesema Ndejembi.
Ndejembi amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipambanua wazi kujali maslahi ya watumishi na ndio imepandisha madaraja watumishi takribani 180,000 mara mbili ya idadi iliyokua imepangwa.
” Hakuna nyakati nzuri kwa watumishi wa umma kama kufanya kazi na Rais Samia fikirieni tulikua tumepanga kupandisha madaraja watumishi 90,000 lakini Rais kwa mapenzi yake akatuelekeza tuongeze idadi kufikia 180,000 huu ni upendo wa hali ya juu ambao kiongozi wetu ameuonesha.
Kwa spidi hii ya Rais Samia na upendo alionao kwa watumishi sisi wasaidizi wake hatutoruhusu Afisa Utumishi ambaye atajaribu kuzuia maslahi ya watumishi, hizi fedha za madai ni haki yao na siyo hisani, shughulikeni madai yao haraka ili watumishi wetu wafanye kazi kwa morali,” Amesema Naibu Waziri Ndejembi.
Aidha Ndejembi amesema katika ajira mpya 34,000 ambazo zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni Serikali itatoa kipaumbele katika kada za Afya na Elimu kwani ndio sehemu ambayo pia Rais Samia ameweka fedha nyingi.
“Rais Samia anafanya kazi kubwa sana fedha ambazo zimeletwa kwenye Halmashauri zetu takribani Sh Trilioni 1.3 zinakwenda kumaliza changamoto ya Madarasa Nchi nzima hadi kwenye Shule Shikizi za Msingi hii haijawahi kutokea hivyo ni lazima tuhakikishe wanapatikana pia Walimu,” Amesema Ndejembi.