Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi Yahaya Njiku (katikati) akikata utepe kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro, kuashiria uzinduzi wa Album ya Kwaya ya Malezi ya Vijana Usharika wa Emanueli Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati Singida juzi.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi Yahaya Njiku (katikati) akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro, katika uzinduzi wa Album hiyo.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi Yahaya Njiku (kushoto) akiwa kwenye hafla hiyo.
Vijana Gospel Choir wakitoa burudani wakati wa uzinduzi huo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Jerry Muro ametoa maombi ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kuliongoza Taifa kwa utulivu na amani.
Hayo yalisemwa juzi kwa niaba yake na Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi Yahaya Njiku katika hafla ya uzinduzi wa Album ya Kwaya ya Malezi ya Vijana Usharika wa Emanueli Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati.
DC Muro alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo lakini kutokana na majukumu mengine aliwakilishwa na Afisa Mtendaji huyu Yahaya Njiku.
” Ndugu zangu niwaombe na kuwasihi wote tuliopo katika hafla hii tuendelee kumuombea Rais wetu Samia Suluhu Hassan aendelee kuliongoza Taifa letu kwa amani na utulivu” alisema Njiku.
Pia Njiku aliwaomba waumini waliokuwepo kwenye hafla hiyo kuiombea Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake kwa jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo na kuhimiza umoja wa kitaifa na kukuza diplomasia na nchi zingine.
Njiku aliwapongeza vijana wa kanisa hilo kwa namna walivyo wa moja kwa kueneza neno la mungu kupitia uimbaji.
Alitumia nafasi hiyo kumshukuru Askofu
Msaidizi wa Kanisa hilo, Katibu Mkuu wa Dayosisi, Mchungaji wa Usharika na viongozi wa usharika hui kwa ujumla katika kushiriki kwao hadi kukamilisha album hiyo.
Uzinduzi huo ulifanyika juzi Jumapili katika Kanisa la KKKT ( Msalaba mrefu) Singida mjini ambapo Vijana Gospel Choir walizindua album yao inayoitwa ‘Wewe ni Mshindi’