Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Uongozi wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) alipofanya ziara katika chuo hicho
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioneshwa ramani ya ujenzi wa jengo la mafunzo la Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) alipofanya ziara chuoni hapo tarehe 29 Novemba 2021. Wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela na Kulia ni Mkuu wa Chuo cha ARIMO Huruma Lugalla.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shighela akizungumza na viongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) waliomtembelea ofisini kwake wakati wa kikao cha Jukwaa la Wahariri kilichofanyika mkoani humo jana. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Morogoro Albert Msando
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt Maulid Banyani (Kulia) akimkabidhi kipeperushi kinachoelezea Mradi wa Nyumba 1000 zinazojengwa na Shirika lake katika mkoa wa Dodoma maeneo ya Chamwino na Iyumbu
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt Maulid Banyani (katikati) akifafanua jambo mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa kutembelea eneo la Kingo Sabasaba Manispaa ya Morogoro kuangalia namna Shirika la Nyumba la Taifa litakavyoweza kufanya uwekezaji eneo hilo.
……………………………………………………….
Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekitaka Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kujipanga na kuhakikisha kinamaliza kazi ya urasimishaji makazi katika maeneo waliyopewa kazi hiyo.
Hatua hiyo inafuatia Naibu Waziri Dkt Mabula kuelezwa na Mkuu wa Chuo cha ARIMO Huruma Lugalla kuwa, moja ya changamoto kubwa katika zoezi zima la urasimishaji makazi maeneo mbalimbali ambayo chuo hicho imechukua kazi hiyo ni kasi ndogo ya uchangiaji gharama kutoka kwa wananchi.
‘’Mhe. Naibu Waziri uchangiaji katika zoezi la urasimishaji makazi katika maeneo mbalimbali nchini tunayoyafanyia kazi hasa hapa Morogoro ni mdogo sana pamoja na gharama ya zoezi hilo kupungua kutoka shilingi 150,000 hadi 130,000/=’’ alisema Lugala
Hata hivyo, pamoja na kuelezwa changamoto, hiyo Dkt Mabula ambaye alikuwa akizungumza na Uongozi wa Chuo cha Ardhi Morogoro tarehe 29 Novemba 2021, alikitaka chuo hicho kuhakikisha kinachukua maeneo machache ya kuyafanyia kazi badala ya kuchukua maeneo mengi aliyoyaeleza kuwa yanaweza kuwashinda kukamilisha kazi kwa wakati.
‘’ Ni vizuri mkajipanga katika zoezi zima la urasimishaji, baada ya kufanyika kosa la awali nyuma sasa msirudie tena kosa maana haitaleta picha nzuri kwa chuo na mnachotakiwa ni kujipanga na kuwa na mkakati wa kukamilisha kazi’’ alisema Dkt Mabula
Mkuu wa koa wa Morogolo Martine Shigela alishangazwa na maelezo kuwa, baadhi ya wananchi katika mkoa wake wanakuwa wazito kuchangia gharama za urasimishaji makazi holela wakati wanaweza kujenga nyumba ya milioni 20 huku akishindwa kuchangia shilingi 130,000/
‘’Yaani wananchi wanashindwa kuchangia gharama za urasimishaji wakati wanajenga nyumba kwa gharama kubwa kama milioni 10 mpaka 20? Hii haina afya kabisa’’alisema Shughela.
Awali Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Huruma Lugalla alimueleza Naibu Waziri Dkt Mabula kuwa Chuo chake kinaendelea na utekelezaji miradi ya urasimishaji makazi katika mitaa 61 nchini kwa kushirikiana na halamashauri na wananchi wanaomiliki ardhi ya makazi yaliyoendelezwa kiholela.
Kwa mujibu wa Lugalla, jumla ya viwanja 30,188 vimeidhinishwa kufanyiwa kazi ya urasimishaji makazi, iwanja 129, 761 vimetambuliwa huku michoro 218 ikisanifiwa na takriban Shilingi Bilioni 2.553 ikiwa imetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Aidha, Mkuu huyo wa Chuo cha ARIMO aliwasilisha ombi la chuo chake kutaka kusaidiwa uendelezaji eneo la ekari 33 lililoko Mlimakola Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kupanua wigo wa mafunzo, miundombinu sambamba na kuongeza udahili wa wanafunzi.
Kufuatia ombi hilo, Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela alisema, ni vyema taasisi za umma zinapoomba msaada wa uendelezaji maeneo yake zikafikiriwa kusaidiwa na kuongeza kuwa, mkoa wake uko tayari kusaidia pale utakapoona mipango ya chuo kuhusu uendelezaji eneo hilo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shighela alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kufikiria namna ya kuwekeza miradi katika mkoa huo ukiwemo ule wa eneo la maduka (MALL) kwa lengo la kurahisisha upatikanani huduma.
Akizungumza na Menijementi ya NHC iliyomtembelea ofisini kwake wakati wa kikao chake na Jukwaa la Wahariri Tanzania mkoani Morogoro kilichofunguliwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, Shighela alisema, kwa sasa mkoa huo hauna maduka (Mall) kwa ajili ya kuwaewezesha wananchi wa mkoa huo kupata huduma eneo moja kama ilivyo Dar es Salaam wakati mkoa huo unaendelea unapanuka.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Numba la Taifa Dkt Maulid Banyani alimhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kulifanyia kazi suala hilo na katika kuhakikisha utekelezaji unafanyika haraka Shigela na timu ya NHC walitembelea eneo la Kingo Sabasaba katika manispaa ya Morogoro kuona namna ya kufanya uwekezaji kwenye eneo hilo.