Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Chunya, Novemba 29, 2021. Kulia. ni Naibu Waziri wa Elimu , Sayansi na Tekinolojia, Omari Kipanga na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Pancras Bujulo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Chunya
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Pancras Bujulo (wa pili kulia) kuhusu ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Chunya baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo hicho, Novemba 29, 2021. Kushoto ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Omari Kipanga na kulia ni Mkuu wa Chuo cha VETA cha Mpanda, Joshua Mategane.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Omari Kipanga (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya VETA, Peter Maduki baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Chunya, Novemba 29, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Muonekano wa Chuo cha Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Chunya ambacho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliweka jiwe la msingi.
………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uamuzi wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi nchini ili wananchi hususani vijana wapate ujuzi na ufundi wa aina mbalimbali utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Novemba 29, 2021) baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha ufundi stadi cha wilaya ya Chunya mkoani Mbeya. Ameagiza ujenzi huo ukamilike kwa wakati ili malengo ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya ufundi chuoni hapo yanafikiwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imeamua kujenga vyuo hivyo vya ufundi stadi ili kufungua milango ya ajira kwa kuwa mafunzo yanayotolewa yatawawezesha wahusika kujiariwa kutika sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda. “Ninawaomba wananchi muendelee kuwa na imani na Serikali yenu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mbeya uhakikishe katika eneo hilo la kijiji cha Mbugani kinapojengwa chuo hicho kunakuwa na huduma zote za kijamii zitakazotosheleza matumizi ya eneo hilo zikiwemo za maji safi na salama na umeme.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia anawasihi wananchi waendelee kuyalinda maeneo yao yaendelee kuwa tulivu ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. “Suala la kuimarisha ulinzi na usalama ni jukumu la wananchi wote, hivyo tuendelee kushirikiana katika kuimarisha ulinzi.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Dkt. Pancras Bujulu amesema mradi huo una jumla ya majengo 17 ambayo ni jengo la utawala, karakana nne, jengo la madarasa, mabweni mawili, bwalo la chakula, majengo matatu ya vyoo, nyumba ya mkuu wa chuo, nyumba ya familia mbili za watumishi, jengo la mitambo ya umeme, jengo la stoo na jengo la walinzi.
Dkt. Bujulu amesema chuo hicho kitakapokamilika kinatarajiwa kuanza na fani sita za muda mrefu, nazo uhazili na kompyuta, ushonaji na ubunifu wa mitindo, uashi, umeme wa majumbani, ufundi magari pamoja na uchomeleaji na uungaji wa vyuma. Amesema gharama za ujenzi wa chuo hicho ni shilingi bilioni 1.6.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa leo Novemba 29, 2021 amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongorosi yenye urefu wa kilometa 39 unaotarajiwa kukamilika tarehe 27 Februari, 2022. Mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 67.2 umegharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.
Baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unaotekelezwa na Mkandarasi China Railway 15 Bureau Group Corporation, ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 98, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wakazi wanaoishi katika maeneo inapopita barabara hiyo watumie fursa ya ujenzi huo kwa kuanzisha miradi itakayowaongezea tija.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mbeya Mhandisi Eliazary Rweikiza amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba 30, 2017 kwa muda wa mkataba wa miezi 46 ambapo ulitarajiwa kumalizika Agosti 31, 2021.
Amesema kuwa hata hivyo Serikali imeongeza mkataba wa ujenzi wa mizani ya kupimia magari inayojengwa katika kijiji cha Matundasi ili kulinda barabara hiyo, hivyo kufanya mradi huo kukamilika ifikapo Februari 27, 2022.