Mkuu wa chuo Cha maendeleo ya jamii Monduli (CDTI)Elibariki Ulomi akizungumza katika maadhimisho hayo wilayani Monduli mkoania Arusha.
………………………………………………..
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Wadau mbalimbali pamoja na jamii wametakiwa kuwa mstari wa mbele kila mmoja kwa nafasi yake kutoa elimu ya kutosha juu ya ukatili wa kijinsia ili kuweza kukomeshwa katika jamii kwani bado ni changamoto kubwa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa chuo Cha maendeleo ya jamii Monduli (CDTI),Elibariki Ulomi wakati akizungumza katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Duniani yaliyoandaliwa na chuo hicho.
Amesema kuwa,siku hiyo inaadhimishwa kuanzia novemba 25 ya kila mwaka ikifuatiwa na siku 16 za mwendelezo ambapo shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na elimu hutolewa ili kuiwezesha jamii kukomesha vitendo vya ukatili katika maeneo yao.
Ulomi amesema kuwa,swala la ukatili wa kijinsia limekuwa ni changamoto kubwa Sana katika jamii huku wanaoathirika na ukatili huo wakiwa ni wanawake,na watoto huku matukio hayo yakiendelea kufumbiwa macho na jamii inayowazunguka .
“Swala hili la ukatili hasa katika jamii ya wafugaji bado ni changamoto kubwa Sana kwani linasababishwa na mila na desturi za jamii hiyo ambapo watoto wa umri wa miaka 16 wamekuwa wakiozwa na kuishia kupata madhara makubwa hasa kipindi cha kujifungua kutokana na wengi wao kutohudhuria kliniki .”amesema Ulomi.
Amesema kuwa,lengo la maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya “Wewe mwananchi komesha ukatili wa kijinsia Sasa,ni kutoa fursa kwa wanawake ,wanaume ,vijana wa kike na kiume na wanaharakati kukuza uelewa wa umma juu ya mchango wa wanawake katika maendeleo .
Naye Mkuu wa kitengo cha dirisha la taarifa kwa wanawake chuoni hapo, Beatrice Kavishe amesema kuwa, hali ya ukatili wa kijinsia wilayani Monduli bado ni changamoto kubwa hasa kwa jamii ya wafugaji ambapo wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii hiyo ya kifugaji kuhusu madhara ya ukatili na kuwapa ushirikiano wa karibu pindi wanapohitajika.
Amesema kuwa,wamefungua kitengo maalumu kwa ajili ya kupokea taarifa za ukatili zinazowahusu wanawake na watoto ambapo zimesaidia Sana kupunguza ukatili wa kijinsia miongoni mwao baada ya kupata elimu hiyo.
“Katika kuadhimisha wiki hii tuna utaratibu wa kutembelea mashuleni kwa ajili ya kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia kwani idadi kubwa ya jamii hiyo bado inaendekeza mila na desturi zao na kuendelea kuwaozesha watoto wakiwa wadogo .”amesema Kavishe.
Naye Daktari wa hospital ya wilaya ya Monduli,Yona Senzota amesema kuwa, swala la ukatili kwa wilaya hiyo bado ni changamoto sana ambapo kwa mwezi wa kumi tu walipata kifo cha binti na mtoto wake kilichosababishwa na mimba za utotoni,huku watoto wachanga wawili wakifariki kutokana na changamoto hiyo ya mimba za utotoni,jambo ambalo bado elimu inahitajika kwa kiwango kikubwa sana.