Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Hassan Pazi ambaye ni fundi mkuu wa kiwanda cha kuchenjua madini ya dhahabu cha Kampuni ya Giant ya Chunya mkoani Mbeya kuhusu uchenjuaji madini ya dhahabu wakati alipotembelea kiwanda hicho, Novemba 29, 2021. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Abdallah Kitwala. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama kazi ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu wakati alipotembelea kiwanda cha kuchenjua madini ya dhahabu cha Kampuni ya Giant ya Chunya mkoani Mbeya Novemba 29, 2021. Kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Abdallah Kitwala. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchenjua madini ya dhahabu cha Kampuni ya Giant ya Chunya mkoani Mbeya Novemba 29, 2021. Aliyekaa kulia ni Naibu Waziri TAMISEMI, Dkt Festo Dugange na kushoto ni Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Omari Kipanga, wa tatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homela, wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya Mchungaji Jacob Mwakasole. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Wanakwaya wa kundi la Agano wakiimba wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowasili kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kipoka wilayani Chunya, Novemba. 29, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia wimbo wa kwaya ya Agano ya Makongorosi baada yakuweka jiwe la msingi la ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sokondari Kipoka wilayani Chunya Novemba 29, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
******************************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara katika sekta ya madini kuuza madini yao katika masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini badala ya kuuza madini hayo katika masoko yasiyo rasmi.
Mheshimiwa Majaliwa amesema hakuna sababu ya kutorosha madini kwani kwa kufanya hivyo nchi inapoteza mapato ambayo yanaiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutoa huduma muhimu za jamii ikiwemo katika sekta za afya, elimu na maji
“Haipendezi sana kwa baadhi ya watu kuendelea na tabia ya kukimbiza dhahabu yetu kwenda kuuza kwenye ‘black market’, Serikali yetu imeweka mazingira mazuri ya uuzaji wa madini, kila wilaya wilaya inayozalisha madini tumeweka masoko tena yanatoa bei nzuri”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 29, 2021) alipotembelea kiwanda cha kuchenjua madini cha ‘Giant Elution’ kilichopo Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.
Baada ya kukagua uwekezaji katika kiwanda hicho ambacho kinamilikiwa na Mtanzania, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa watanzania kuendelea kuwekeza katika sekta ya madini kwani Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji imeweka mazingira bora kwa wawekezaji wazawa.
“Maafisa wa Madini hakikisheni mnawatembelea wachimbaji wadogo, muwaelimishe pamoja na kuwawezesha kupata fursa katika taasisi za kifedha ili waweze kupata mikopo itakayo wawezesha kununua vifaa vya kisasa na kuongeza tija katika uchimbaji wao.”
Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na taarifa ya Wilaya ya Chunya kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato katika sekta ya madini na kuwapongeza viongozi wa Wilaya na Mkoa kwa kuwa na usimamizi mzuri pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Juma Homera, Amesema Mkoa wa Madini wa Chunya kwa mwezi walikuwa wanakusanya kilo 20 kwa mwezi lakini baada ya masoko kuanza wanakusanya kilo 250 hadi 300 ambayo hadi sasa wamekusanya tani 6.4 yenye thamani ya shilingi bilioni 719.6.
“Serikali imepata zaidi ya shilingi bilioni 43.2 kama sehemu ya mrahaba na shilimgi bilioni 7.2 kama ada ya ukaguzi ambapo jumla Serikali imepata shilingi bilioni 50.3”.
Awali akifanya ukaguzi wa ujenzi wa madarasa saba katika Shule ya Sekondari Kipoka iliyoko Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya, Waziri Mkuu ameziagiza Mamlaka zinazohusika na usambazaji wa maji nchini ikiwemo RUWASA kuhakikisha zinafikisha huduma ya maji katika taasisi zote za serikali ikiwemo, Shule, Vituo vya Afya, pamoja na maeneo mengine ya huduma za kijamii.