Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Petro Lyatuu akizungumza na ujumbe wa wataalamu kutoka nchini Malawi uliokuja nchini kwa ajili ya kujifunza kuhusu kuanzishwa kwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na utekelezaji wa majukumu yake.
Washiriki kutoka Wakala wa Umeme Vijijini (REA) wakifuatilia kwa makini maelekezo mbalimbali yaliyokuwa yanatolewa na Kaimu Mkurugenzi wa REA Mha.Jonas Olotu(hayupo pichani)
Ujumbe wa wataalamu kutoka nchini Malawi uliokuja nchini kwa ajili ya kujifunza kuhusu kuanzishwa kwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na utekelezaji wa majukumu yake ukifuatilia kwa makini maelekezo yaliyokuwa yakitolewa kwao.
***********************
Tanzania imepokea ujumbe wa wataalamu kutoka nchini Malawi kwa ajili ya kujifunza kuhusu kuanzishwa kwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na utekelezaji wa majukumu yake nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Bw. Petro Lyatuu wakati akizungumza na ujumbe kutoka nchini Malawi uliojumuisha wataalamu kutoka Wizara za Nishati na Fedha uliokuja nchini kujifunza kuhusu wakala huo.
“Tangu kuanzishwa kwa REA mwaka 2007, wakala umekuwa ukitekeleza majukumu yake na kipindi hicho wenzetu wa Malawi wamepata taaarifa mbalimbali kuhusu wakala na mafanikio ambayo wakala umeyapata kwa kipindi hicho na wameona ni vyema wakaja nchini Kwetu ili kujifunza kuhusu kuanzishwa kwake, changamoto na mafanikio yake” amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa REA Mha.Jonas Olotu amesema wakala huo uko tayari kuisaidia nchi ya Malawi katika kuipa ujuzi,maarifa ili ifanikiwe katika kuanzisha Wakala wa Umeme Vijijini nchini kwao. Ameongeza kuwa sio tu nchi ya Malawi pekee ambayo imekuja kwa ajili ya kujifunza kuhusu masuala haya ya umeme vijijini bali nchi kama Lesotho nao walikuja na wakapata msaada kama huo.
“Kwa kweli tumefurahi kwa ujio wao na tungependa wafanikiwe hata zaidi yetu kwa kuanzisha wakala wao kwani tungependa kuwa sehemu ya mafanikio yao, hizi ni jitihada kubwa za Serikali kuweza kuziwezesha Taasisi zake ambazo sasa zinaonesha mfano mkubwa na kuiletea sifa kwa maana ya maendeleo ambayo tumeyafanya” amesema.
Naye Naibu Mkurugenzi kutoka Wizara ya Nishati nchini Malawi Patrick Silungwe amesema wameichagua Tanzania kuja kujifunza kwa sababu ina mafanikio makubwa katika eneo hilo.
“Sisi kama nchi ya Malawi tumekuwa tukitekeleza katika masuala haya ya umeme vijijini kwa muda sasa Serikalini ,lakini baada ya kupata misukosuko ya hapa na pale tukaona ni vyema sasa tuanzishe wakala wa umeme vijijini kama nchi,kwaiyo tulihitaji nchi ambayo tayari ni mfano katika masuala haya ya umeme vijijini na hivyo Tanzania ikajitokeza ya kwanza katika orodha yetu na hivyo tumejifunza vyema na tutaenda kutumia maarifa haya kuanzisha wakala wa umeme kutokana na tulichopata Tanzania”ameongeza.