**************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
SHULE ya awali na msingi ya Glisten ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, iliyoshika nafasi ya 15 kwa ufaulu wa darasa la saba kitaifa imetakiwa isibweteke na mafanikio hayo ila iongeze juhudi ili kutangaza eneo hilo lenye madini ya Tanzanite.
Katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka huu shule hiyo imekuwa ya kwanza kwenye mji mdogo wa Mirerani, ya kwanza katika Wilaya ya Simanjiro, ya kwanza Mkoani Manyara na ya 15 kitaifa kwa ufaulu.
Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo ameipongeza shule hiyo kwenye mahafali ya kwanza ya darasa la saba ya shule ya msingi Glisten, iliyoshika nafasi ya 15 kitaifa kati ya shule 5,664 kwa ufaulu wa darasa la saba mwaka huu.
Kobelo amesema kuna shule za binafsi zenye kutoa elimu kwa gharama kubwa nchini na hazikufanikiwa kushika nafasi hiyo ila Glisten imeweza na inapaswa iongeze juhudi zaidi.
“Glisten mmetutoa kimasomaso Mirerani kwani hivi sasa tunazidi kutangazika kwa mazuri tofauti na miaka iliyopita nazipongeza na shule nyingine za Mirerani pia zilizofaulisha vizuri,” amesema Kobelo.
Amesema wadau wengine wa maendeleo waige mfano wa Diwani mstaafu wa kata ya Mirerani, Justin Nyari kwa kuwekeza kwenye jamii kupitia shule hiyo kuliko kuwekeza mikoa mingine.
Mkurugenzi wa shule ya awali na msingi Glisten, Justin Nyari ambaye pia ni mchimbaji na mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, amewashukuru wazazi na walezi kwa kuiamini shule hiyo na kuwasomesha watoto wao kwenye shule hiyo.
Nyari amesema kuwa na shule ni jambo moja na kuwa na wanafunzi ni jambo lingine hivyo wazazi, Walimu na wanafunzi wanastahili lililobora na pongezi nyingi kupitia mahafali hayo.
“Namshukuru Mungu kwa uwezo huu kwani siyo jambo dogo kwa shule ambayo inafanya mahafali kwa mara ya kwanza kuwa ya kwanza kiwilaya, ya kwanza kimkoa na ya 15 kitaifa,” amesema Nyari.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Mhe Lucas Chimbason Zacharia ameipongeza shule hiyo kwa hatua hiyo na kuwataka waongeze juhudi ili mwakani washike nafasi kubwa zaidi ya hiyo kitaifa.
Amesema kiwango cha taaluma cha shule hiyo ni kikubwa kwani wamewaona wanafunzi wanavyoeleza somo la sayansi ipasavyo ikiwemo moyo unavyofanya kazi.
Mkurugenzi wa shule hii tunakupongeza kwani umezaliwa Mirerani, ukasoma shule ya msingi Mirerani na ukawekeza shule nzuri ya Glisten unastahili pongezi,” amesema mhe Luka.
Mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi Glisten, Sabato Joshua amesema ushirikiano wa mkurugenzi wa shule hiyo, walimu, wazazi, walezi na wanafunzi, umesababisha ushindi huo.
Mwalimu Sabato amesema pia wanafunzi hao baada ya kumalizia silabasi ya msimu mmoja walianza kufundishwa silabasi ijayo hivyo kuelewa vyema masomo yao.
Mwanafunzi wa darasa la tatu wa shule hiyo, Abubakary AbdulRahman alikuwa kivutio kwenye mahafali hayo kwa kutaja miji yote mikuu ya nchi za Africa.
Pia wimbo wa kuagana wa wanafunzi hao wa darasa la saba ulitoa simanji na wengine machozi kuwatoka kutokana na wao kufikia hatua hiyo.