Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka Meneja Mkuu wa kiwanda cha maji cha Tukuyu Spring Water, Godfrey Ng’wanang’walu kuhusu uzalishaji wa maji wakati alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Kibisi, Tukuyu mkoani Mbeya
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary Majaliwa wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kiwanda cha maji cha Tukuyu Spring Water kilichopo Kibisi, Tukuyu mkoani Mbeya baada ya kutembelea kiwanda hicho, Novemba 27, 2021. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homela na kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Mchungaji Jacob Mwakasole.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary Majaliwa wakiagana na wafanyakazi wa kiwanda cha maji cha Tukuyu Spring Water baada ya kutembelea kiwanda hicho eneo la Kibisi Tukuyu mkoani Mbeya, Novemba 27, 2021. (Picha na Ofisi ya Wziri Mkuu)
……………………………………………………
TUTAENDELEA KUWASAIDIA WAWEKEZAJI NA WAFANYABIASHARA – MAJALIWA
WAZIRI MKUU, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa maelekezo kwa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kuwasaidia wawekezaji pamoja na wafanyabiashara wadogo ili wafanye vizuri katika shughuli zao kwa kuwa kuna faida kubwa kwa Taifa.
“Haya ni maelekezo thabiti ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa ni lazima sekta zote zinazohusika na uwekezaji, ziendelee kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Novemba 27, 2021) alipotembelea kiwanda cha maji cha Tukuyu Springs Water Limited, Kilichopo katika Kijiji cha Kibisi, Kata ya Kyimo, Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya.
Mheshimiwa Majaliwa amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) itaendelea kuboresha mazingira bora ya uwekezaji na kushughulikia changamoto zinazowakabili pamoja na kutoa fursa kwa wawekezaji wazawa.
“Serikali inaendelea kuboresha miundombinu yote muhimu kwa wawekezaji ikiwemo, kuweka mfumo rahisi wa kuwapatia wawekezaji ardhi, kuboresha miundombinu ya barabara, nishati na maji”
Amesema uwekezaji hasa wa wazawa umekuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania kwani wanaelewa mazingira halisi ya maeneo wanayowekeza huku akipongeza kitendo cha kiwanda hicho cha Tukuyu Springs Water Limited kuwawezesha wakazi wanaozunguka eneo la kiwanda kupata huduma ya maji safi na salama pamoja na kuwasaidia kuunganishiwa huduma ya umeme.
Waziri Mkuu pia amewahakikishia wawekezaji kuwa Watanzania wengi sasa wana elimu ya kutosha na utaalam wa kuajiriwa na wanaaminika katika maeneo yao ya kazi na hilo limedhihirishwa na muwekezaji wa kiwanda hicho kwa kuajiri asilimia 100 ya Watanzania na kazi zinafanywa vizuri na kiwanda hicho kimepata mafanikio.
Awali akitoa taarifa ya uwekezaji Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Godfrey Ng’wanang’walu ameishukuru Serikali kwa mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa kwa wawekezaji wazawa na ameahidi kuendelea kuwekeza zaidi na kutoa ajira kwa Watanzania “Kwa sasa kiwanda kiko katika hatua ya upanuzi ili kuongeza uzalishaji”.
“Uwekezaji huu ni matunda ya mazingira bora yaliyotengenezwa na nchi yetu, tumekuwa na mafanikio katika kipindi chote cha uzalishaji na tumeweza kulipa kodi kwa uaminifu mkubwa, katika kipindi chote tumepata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya, sisi tutaendelea kuwekeza zaidi”.